Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola amewaonya Polisi nchini ambao wanatumiwa na mafisadi kuwanyanyasa wananchi maskini kwa kupora ardhi zao na kukimbilia kufungua kesi vituoni wakilazimisha ardhi hiyo iwe mali yao.

Ametoa onyo hilo wakati akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika Kijiji cha Ragati, Kata ya Kasuguti, Jimbo la Mwibara, wilayani Bunda, Mkoa wa Mara.

Amesema kuwa amepata malalamiko mengi kutoka sehemu mbalimbali nchini, kuwa mafisadi huonea wananchi maskini kwa kupora kwa nguvu ardhi wakidai wanamiliki wao na wanatumia badhi ya polisi wasiokuwa waaminifu ili kuwakandamiza wananchi hao.

Aidha, Lugola amepiga marufuku kwa mwananchi yeyote ambaye anakurupuka kukimbilia kituo cha polisi kufungua kesi za ardhi ambazo hazina uthibitisho wa jinai yoyote, badala yake kesi au malalamiko yake kwanza ayapeleke katika mabaraza ya ardhi.

“Kuanzia sasa mwananchi yeyote atakayeenda kufungua kesi kituo cha polisi inayohusu masuala ya ardhi na endapo kiwanja hicho kimepimwa lazima awe na hati inayoonyesha yeye ni mmiliki halali, ili iwasaidie polisi wajue wewe ndio mmiliki halali,”amesema Lugola

Hata hivyo, Lugola ameongeza kuwa, hataki kusikia mwananchi anaonewa, na pia aliapa hatacheka na mafisadi, atapambana nao sehemu yoyote nchini na pia yupo tayari kwa lolote na  ameanza kupambana na mafisadi ndani ya wizara yake na tayari wameanza kurudisha fedha za Serikali.

 

Jeshi la Polisi lasweka ndani Kijiji kizima Mbeya
Dkt. Bashiru awafunda UVCCM