Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola amepiga marufuku tabia ya baadhi ya askari, polisi kutoza fedha kwa ajili ya huduma ya dhamana kwa watuhumiwa waliopo mahabusu katika vituo vya polisi nchini na kukemea utaratibu wa watuhumiwa kunyimwa dhamana hasa siku za mapumziko kwa kisingizio kuwa si siku za kazi.

Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji cha Busanza wilayani Uvinza mkoani Kigoma, Lugola amesema dhamana kwa mtuhumiwa inapaswa kutolewa saa 24 na siku zote za wiki.

Amesema vituo vya polisi nchini vinafanya kazi siku zote za wiki zikiwemo za mapumziko, hivyo amepiga marufuku kwa askari yeyote kushindwa kutoa dhamana kwa kosa lenye dhamana.

”Hii tabia sijui imetoka wapi, ambayo imejengeka kwa baadhi ya askari polisi, Eti mtu akiingia mahabusu ya polisi siku ya ijumaa, siku ya jumamosi na jumapili, hawatoi dhamana wakisema dhamana mpaka jumatatu, hii tabia sio sahihi na ife haraka iwezekanavyo”amesema Lugola.

Ameongezea kuwa kunatabia ambayo imezoelewa katika jamii, kuingia polisi ni bure ila kutoka ni fedha, hii kauli nataka ife, kwa sababu nawajua polisi na hawanidanganyi kwa lolote hivyo ole wao ambao watawanyanyasa wananchi kuwaomba fedha”.

Lugola amesisitiza kuwa dhamana ni haki ya mtu endapo hilo kosa linadhaminika, hivyo mwananchi yeyote atakaeombwa fedha anapaswa kuripoti tukio hilo kwa viongozi wa polisi ili polisi achukuliwe hatua za kinidhamu

 

Afrika kumpigia kura Gianni Infantino
Ndoa ya Lulu yaiva, avishwa pete