Mshambuliaji kutoka nchini Uruguay Luis Suarez amempa ushauri wa bure Ousmane Dembele, kwa kumwambia hana budi kuiga mazuri kutoka kwa wachezaji wenzake wa FC Barcelona, ili kuondokana na kadhia inayomsibu katika kipindi hiki.

Dembele amekua na wakati mgumu wa kurekebisha nidhamu yake, jambo ambalo linatajwa kuwa msukumo mkubwa kwa meneja wa Barca Ernesto Valverde kuomba mshambuliaji huyo auzwe itakapofika mwezi Januari 2019.

Dembele hakua sehemu ya kikosi kilichocheza mchezo wa ligi ya Hispania dhidi ya Real Betis, waliochomoza na ushindi wa mabao manne kwa matatu majuma mawili yaliyiopita, kutokana na kushindwa kujumuika na wenzake kwenye mazoezi kwa kipindi cha siku tatu.

Akizungumza kabla ya mchezo wa kimataifa wa kirafiki kati ya Uruguay na Ufaransa uliochezwa mjini Paris, Suarez amesema mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 21, kama hatokua tayari kubadilika ataendelea kuwa kwenye wakati mgumu wa kutimiza ndoto zake za kucheza soka la ushindani kwenye kikosi cha kwanza cha Barcelona.

“Anahitaji kuangalia sana mipango na mikakati yake binafsi, kisha ajitathmini yupo kwenye klabu ya aina gani, akifanya hivyo itakua rahisi kwake kubadilika kwa haraka na kurejea kwenye soka la ushindani.” Alisema Suarez.

“Ni vigumu kwa kila mmoja kukubali kwa urahisi maisha ya mchezaji kama Dembele anayoishi kwa sasa, kila mmoja hakubaliani na anachokifanya, kwa sababu hakutegemewa kufanya haya, lakini ninamaini bado ana muda wa kubadilika na kurejea katika kiwango chake kizuri.”

Dembele bado hajaonyesha uwezo wake kisoka tangu alipotua FC Barcelona akitokea Borussia Dortmund mwaka 2017, na haijafahamika nini kinachomsibu hadi kufikia hatua ya kuonyesha utovu wa nidhamu.

Usajili wake uliigharimu FC Barcelona Euro milioni 105 sawa na dola za kimarekani 119.01, akichukua nafasi iliyoachwa wazi na mshambuliaji kutoka Brazil Neymar, aliyetimkia PSG.

Majaliwa awataka wananchi kumcha Mungu
Video: Dkt. Bashiru Ally afunguka kuhusu vyama vya siasa kutoshirikiana