Kiungo wa klabu bingwa barani Ulaya Real Madrid Luka Modric, amemtaka Neymar kujiunga naye Santiago Bernabeu msimu ujao wa ligi, ili kuendeleza mazuri ya klabu hiyo.

Modric aliwasilisha ombi hilo kwa Neymar, wakati wa mchezo wa kimataifa wa kirafiki kati ya Brazil na Croatia uliofanyika jana mjini Liverpool, England.

Kiungo huyo kutoka Croatia, alitumia nafasi ya kufikisha ujumbe kwa Neymar, wakati wakibadilishana jezi, mara baada ya dakika 90 za mchezo huo kufikia kikomo, huku Brazil wakuibuka na ushindi wa mabao mawili kwa sifuri.

Wakati wa tukio hilo Modric alionekana akimwambia jambo mshambuliaji huyo wa Brazil, na tukio hilo lilipofuatiliwa na wataalamu wa kusoma alama za midomo wamegundua alichokizungumza.

Imebainika Modric alisema “Tunakusubiri. ”  Na baadae wawili hao walicheka na kutabasamu kwa pamoja.

Neymar anaeitumikia klabu ya Paris St Germain, jana alirejea kwa mara ya kwanza uwanjani baada ya kupona majeraha ya mguu, na kufanikiwa kufunga bao la kwanza la Brazil na kubua hisia upya kwa kwa mashabiki wake waliokua na hamu ya kumuona tena uwanjani, baada ya majuma kadhaa.

Neymar, alijiunga na PSG mwaka 2017 kwa ada ya Euro milioni 222 sawa na Pauni milioni 259, na sasa anahusishwa na taarifa za kutaka kujiunga na wapinzani wa klabu yake ya zamani FC Barcelona (Real Madrid).

Gazeti la Marca la nchini Hispania limewahi kuripoti kuwa, baba mzazi wa mshambuliaji huyo Neymar Sr, ambaye pia ni wakala wake, amewaambia viongozi wa PSG mwanae anataka kuondoka, huku akihusishwa kufanya mazungumzo na wakurugenzi wa Real Madrid mjini Paris mwezi Disemba mwaka 2017.

Rais wa klabu ya Real Madrid Florentino Perez aliwahi kujinasibu hadharani kwa kusema, walijaribu kumsajili Neymar kabla ya kujiunga na Barca mwaka 2013, na bado ana kiu ya kumuona Mbrazil huyo akicheza katika himaya ya klabu yake.

Msimu wa 2017/18 Neymar alifanikiwa kufunga mabao 28, na kutoa pasi za mwisho 16 katika michezo 30 aliyocheza katika michuano yote akiwa na klabu ya PSG, kabla ya kuumia mguu Februari 25.

LIVE: Rais Magufuli akizinduzi Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo awamu ya Pili
Kocha Age Hareide amtema Nicklas Bendtner