Mshambuliaji kutoka nchini Ubelgiji na klabu ya Everton, Romelu Menama Lukaku, amewasilisha salamu kwa mahasimu wao wakubwa, Liverpool FC baada ya kufanya kazi ya ziada usiku wa kuamkia hii leo.

Lukaku, alifunga mabao mawili muhimu katika mchezo wa ligi ya nchini England baada ya The Toffees kuwa nyuma kwa mabao mawili dhidi ya West Brom, ambao walikwenda mapumziko wakiongoza.

West Brom, walipata mabao hayo mawili ya kuongoza kupitia kwa mshambuliaji wao hatari Saido Berahino pamoja na Craig Dawson na waliamini mambo yalikua yamewanyookea.

Lukaku aliwatia shime wachezaji wenzake wa Everton dakika 10 baada ya kuanza kwa kipindi cha pili, kwa kufunga bao la kwanza huku mshambuliaji kutoka nchini Ivory Coast, Arouna Kone akifunga bao la kusawazisha katika dakika ya 76.

Lukaku, alirejea tena langoni mwa West Brom na kufunga bao la tatu lililowapa ushindi Everton katika dakika ya 84, na kuwapa nafasi mashabiki pamoja na vyombo vya habari kumzungumza kwa kina na kuamini huenda akawa mwiba mkali kwa mahasimu wao Liverpool mwishoni mwa juma hili, watakapokutana kwenye uwanja wa Goodson Park.

Everton wamekua na upinzani wa kihistoria dhidi ya Liverpool kutokana na uhasama wa kisoka uliojengeka baina ya klabu hizo mbili ambazo zina maskani yake makuu mjini Liverpool.

Kwa ushindi wa mabao matatu kwa mawili uliopatikana usiku wa kuamkia hii leo, Everton wamejisogeza katika nafasi ya tano kwenye msimamo wa ligi ya nchini England kwa kufikisha point 12, huku Liverpool ambao walishinda mchezo wao wa mwishoni mwa juma lililopita wakishika nafasi ya 9 kwa kumiliki point 11.

Jack Grealish Aitosa Ireland Ya Kaskazini
Video: Lowassa Umemsikia Nape?