Mwendo wa kutumbua majipu unaendelea kutekelezwa na mawaziri wa serikali ya awamu tano na umeligusa jengo refu lililoko katika mtaa wa Indira Ghandhi jijini Dar es Salaam ambalo limebainika kujengwa chini ya kiwango.

Jengo hilo limekuwa likilalamikiwa na wananchi wanaokaa katika maeneo hayo kuwa kadri linavyozidi kujengwa, linaathiri majengo yaliyoko katika maeneo hayo na kusababisha kutengeneza nyufa.

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi ameiagiza Halmashauri ya Manispaa ya Ilala pamoja na Shirika la Nyumba la Taifa kuhakikisha wanalibomoa jengo hilo ndani ya kipindi cha mwezi mmoja.

Lukuvi alieleza kuwa Rais Mstaafu, Jakaya Kikwete alifika katika eneo hilo miezi sita iliyopita na kuagiza jengo hilo libomolewe, lakini watendaji hao wameendelea kufumbia macho ujenzi wa jengo hilo.

Ghorofa

“Miezi sita iliyopita Rais Mstaafu alikuja hapa akaagiza jengo hili libomolewe na nyie mkajiridhisha kweli lafaa kubomolewa sasa inakuwaje mpaka leo linaendelea kuwepo? Naagiza mfanye haraka jengo hili ndani ya mwezi mmoja taratibu za ubomoaji ziwe zimeanza ili kulinusuru taifa kuingia katika janga jingine.”alisema Waziri Lukuvi.

Jengo hilo limeonekana kutengeneza nyufa kubwa wakati bado linaendelea kujengwa, hali inayohatarisha usalama wa wananchi.

 

 

 

Membe akaribishwa Chadema
Rihanna awaandaa mashabiki kula ‘ANTI’ baada kukamilisha mapishi