Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, amewataka viongozi wa mabaraza ya ardhi kuhakikisha wanatenda haki kwa wananchi na kuepuka rushwa inayodaiwa kukithiri kwenye eneo hilo.
Ameyasema hayo alipokuwa akizindua jengo la Baraza la Ardhi na Nyumba Mkoa wa Kigoma ambapo amesisitiza kufanya kazi kwa uzalendo na weledi.
Lukuvi amesema mabaraza mengi ya ardhi yamekuwa yakiwaonea wananchi na kuwanyima haki wale wanaostahili kupata haki hiyo, pia ametanabaisha kuwa kitu kikubwa kinacho waumiza wananchi ni pamoja na tatizo la ardhi, ambapo ameyataka mabaraza hayo kuacha mara moja tabia ya kudai rushwa kwa wananchi wanaofika kuomba msaada wa kupatiwa haki yao.
Ameongeza kuwa mabaraza hayo yanapaswa kufanya kazi kwa haki na kuhakikisha hayamwonei mwananchi masikini hata mmoja kwa kutumia madaraka waliyonayo.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Bregadi Jenerali Mstaafu Emamanuel Maganga, aliyaomba mabaraza hayo kutoa hukumu mapema ili wale watakaoshindwa kukubaliana na uamuzi uliotolewa waweze kukata rufani na kutafuta haki kwenye ngazi zingine.