Muigizaji wa kike na mshindi wa tuzo ya Oscars, Lupita Nyong’o amewaomba radhi watu wenye ulemavu wa sauti kutokana na jinsi alivyocheza kwenye filamu yake mpya ya kutisha iitwayo ‘Us’.

Lupita aliwatibua watu wenye ulemavu wa sauti unaofahamika kwa lugha ya kitaalam kama Disorder Spasmodic dysphonia (SD) ambao umewahi kuwapata watu maarufu kama Robert F Kennedy, baada ya kusema kuwa uhusika wake kwenye filamu hiyo kama ‘Red’ mwenye tatizo la sauti ulitokana na kuvutiwa na jinsi Robert F. Kennedy alivyokuwa akizungumza.

Kauli hiyo ilitafsiriwa kama kejeli kwa watu wanaoishi na ulemavu huo. Taasisi ya walemavu wa Spasmodic dysphonia ya Marekani iitwayo National Spasmodic Dysphonia Association ilitoa tamko la kulaani maelezo ya Lupita ambayo aliyatoa kwenye mahojiano na ‘View’.

“Sauti ya pasmodic dysphonia sio sauti ya kutisha, sio sauti ya kuchekesha, ni ulemavu ambao watu wanaishi nao na hawapaswi kuhukumiwa kwa hilo,” lilieleza tamko hilo.

Tamko hilo lilieleza kuwa kitendo cha kuonesha mtu mwenye ulemavu huyo kama mtu hatari na muovu kama ilivyotokea kwenye filamu ya ‘Us’, ni kuwakosea watu hao ambao nao pia wanataka kutoa mchango wao kwa jamii.

Wikendi iliyopita, muigizaji huyo wa kike ambaye ni raia wa Kenya, aliomba radhi na kueleza kuwa hakuwa na maana ya kuwaudhi watu wenye ulemavu huo.

“Fikra zilizoibuliwa kwa namna hiyo, haikuwa nia yangu. Katika akili yangu, sikuwa nataka kuwaumiza au kuwaonesha vibaya watu wenye changamoto hiyo. Naomba mnisamehe kama nimewakwaza,” alisema Lupita Nyong’o.

Filamu ya Us ambayo ilizinduziwa Machi 22mwaka huu nchini Marekani, imepata mafanikio makubwa ikivunja rekodi ya kuwa filamu ya kwanza ya kutisha nchini Marekani kuingiza $70 milioni kwa pato la wikendi.

Live: Rais Magufuli akiweka jiwe la msingi katika uwanja wa ndege Mtwara
Kanda ya Pwani kuneemeka na mradi wa maji wa Sh14 bilioni