Rapa wa Nigeria, M.I Abaga na lebo yake ya Chocolate City wamefungua mashitaka dhidi ya gwiji wa rapa kutoka Marekani, Nas ambaye jina lake halisi ni Nasir Jones, kwa madai ya kushindwa kuwapa ubeti (verse) ingawa walimlipa.

Kwa mujibu wa mashtaka yaliyofunguliwa kwenye Mahakama ya Juu jijini New York, M.I na lebo yake wanadai kuwa mwaka 2013, walimlipa Nas kiaisi cha dola za kimarekani elfu 50 ($50,000) ili aweze kuwatumia ubeti kwa ajili ya wimbo wa rapa huyo wa Nigeria, lakini hakufanya kama walivyokubaliana.

M.I ameeleza kuwa ingawa Nas alituma ubeti kwa ajili ya M.I, walipousikiliza walibaini kuwa haukufuata makubaliano yao kwani haukuwa na maneno ambayo walikuwa wamemuelekeza pamoja na kuwa tofauti na somo la wimbo husika.

Maneno ambayo walikubaliana yawe sehemu ya ubeti wa NAS ni pamoja na, “M.I, Chocolate City, Nigeria, Queens – New York (Jiji analotoka NAS), Mandela, Trayvon Martin, na mahangaiko ya Waafrika na Wamarekani Weusi.”

Lebo ya Chocolate wameeleza kuwa walikubaliana tena na NAS kupitia wakala wake waliyemtaja kama Goodman kuwa angerudia ubeti huo na kuwatumia kwa wakati.

Hata hivyo, imepita miaka minne bila majibu yoyote kutoka kwa NAS huku wimbo wa M.I uliokuwa unasubiri sauti ya gwiji huo ukiendelea kusota studio, na lebo hiyo kupoteza kiasi hicho cha fedha.

Katika maelezo yao kwenye hati ya mashtaka, M.I na Chocolate City wamemsifu NAS wakimtaja kuwa ‘rapa na mwandishi wa mashairi mwenye heshima ya juu zaidi kwenye kiwanda cha muziki’ na kwamba walitaka ubeti wake kutokana na ‘kipaji chake cha kipekee cha kughani’.

Wanasema cha kushangaza sifa hizo hawakuziona kwenye ubeti wake waliotumiwa. Hivyo, wanaiomba mahakama imuamuru Nas kuwapa ubeti wenye vigezo walivyokubaliana.

‘Produza’ ajibu tuhuma za kumnyanyasa Lupita Kingono
Trump kuamuru siri ya mauaji ya 'Rais Kennedy' kuwekwa hadharani