Serikali imewataka Wakuu wa Mikoa kuhakikisha elimu ya kina inatolewa kwa wananchi juu ya haki, ulinzi, usalama na ustawi wa wazee na kwamba utekeleza wa mkakati wa Kitaifa wa Kutokomeza Mauaji kwa Wazee unaendelea.

Wito huo, umetolewa hii leo Juni 7, 2023 na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima wakati akizungumza na wajumbe wa Baraza la Wazee kata ya Mkonze, Mkoani Dodoma kuelekea Siku ya Kupinga Ukatili dhidi ya Wazee inayofanyika Juni 15 kila mwaka.

Amesema, kutokana na kuboreshwa kwa huduma za kijamii nchini idadi ya wazee imeongezeka kutoka 2,507,568 hadi kufikia 5,008,339 ambayo ni sawa na asilimia 8.1 ya Watanzania 61,741,120 na kwamba katika Maadhimisho hayo ni muhimu kuuhabarisha umma juu ya mambo hayo.

Amesema, “ninachukua fursa hii pia kuwaomba Wakuu wa Mikoa yote nchini kuratibu maadhimisho haya kimikoa kwa kushirikiana na viongozi wa Mabaraza ya Wazee katika mikoa husika, tunapoelekea Siku ya  maadhimisho hayo.”

Hata hivyo amesisitiza, jamii yote kuacha kufanya ukatili kwa Wazee na makundi yote kwa ujumla na amewaomba Wanahabari kutumia kalamu zao kuelimisha na kuendelea kukemea masuala ya ukatili nchini kote na kwamba Serikali itaendelea kuwashughulikia wale wote watakaobainika kufanya vitendo vya ukatili kwa makundi mbalimbali katika jamii hususani kwa wazee.

Maadhimisho ya Kupinga ukatili Dhidi ya Wazee mwaka huu yatafanyika katika ngazi ya Mikoa kote nchini yakiwa na Kaulimbiu ya “Wazee Wanastahili Heshima na Usikivu Wetu”.

Kiungo AS Bamako amvulia kofia Fiston Mayele
Vinicius Junior awapeleka jela mashabiki Hispania