Mchezo wa ligi kuu ya Vodacom mzunguuko wa 11 kati ya Yanga dhidi ya Prisons umemalizika kwa timu hizo kutoka sare ya bao 1-1.

Licha ya kutawala mchezo huo kwa muda mwingi Yanga imeshindwa kuibuka na ushindi ambao ungeiwezesha kupanda kileleni mwa msimamo wa ligi.

Prisons ilikuwa ya kwanza kupata bao la kuongoza kwenye dakika ya 10 baada ya mshambuliaji Eliut Mpepo kuwazidi ujanja mabeki wa Yanga na kuutumbukiza mpira wavuni kirahisi.

Kuingia kwa bao hilo kuliiamsha Yanga iliyosaka bao ka kusawazisha huku Prisons ikijilinda kwa muda mwingi na kutumia mashamulizi ya kushitukiza.

Kwenye dakika ya 37, Lambert Sabianka wa Prisons alitolewa nje kwa kadi nyekundu baada ya kujaribu kumpiga kiwiko Juma Abdul wakati wakigombea mpira wa juu.

Kamera za televisheni ya Azam zilinasa tukio hilo ambalo mwamuzi alilibaini na kuchukua maamuzi ya kufuata sheria 17 za FIFA kwa kumtoa nje Sabianka.

Juhudi za Yanga zilizaa matunda kwenye dakika ya 42 baada ya Raphael Daudi kusawazisha akipokea pasi kutoka kwa Obrey Chirwa.

Kipindi cha pili ni Yanga iliyokuwa ikishambulia mda wote huku Prisons ikipaki basi kusaka sare.

Katika dakika ya 52 Obrey Chirwa alifunga bao ambalo hata hivyo lilikataliwa na mwamuzi kwenye mazingira ya kutatanisha akimtuhumu mfungaji alikuwa ameotea.

Hata hivyo mpira uliokuwa umepigwa na Pius Buswita uliguswa na mlinda lango wa Prisons kabla haujamfikia Chirwa.

Mashambulizi mengi ya Yanga hayakuzaa matunda kutokana na uimara wa safu ya ulinzi ya Prisons waliokuwa wakizuia wote.

Wakati mpira huo ukielekea ukingoni Chirwa alikosa nafasi nyingine mbili za wazi moja akipaisha mpira akiwa hatua tatu tu kutoka langoni huku mpira wake mwingine ukigonga mwamba kwenye dakika za majeruhi.

Matokeo hayo yameifanya Yanga iendelee kubakia nafasi ya tatu baada ya kushindwa kuzionoda kileleni Simba na Azam ambazo zinacheza kesho na keshokutwa.

Matokeo ya michezo mingine

Karia atuma salamu za rambirambi msiba wa Gama
Waziri Mwakyembe kuzindua ligi ya wanawake Arusha