Uongozi wa timu ya Ruvu Shooting umesema kwamba, timu yao haipo tayari kucheza mchezo wa ligi kuu kesho dhidi ya Yanga endapo Bodi ya Ligi/ TFF watashikilia msimamo wao wa mchezo huo kuchezwa kesho katika uwanja wa Uhuru, Dar es salaam.

Maamuzi hayo yamefikiwa na uongozi wa timu chini ya Mwenyekiti wake Kanali Charles Mbuge muda mfupi baada ya timu hiyo kuwasili Mlandizi saa 4.15 asubuhi ya leo, Novemba 8,2016 ikitokea Kagera ambapo Jumapili iliyopita, Novemba 6, 2016 ilicheza na Kagera sugar katika uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba.

Mwenyekiti wa timu hiyo, Kanali Mbunge alisema, katika hali ya uchovu waliyonayo wachezaji baada ya kusafiri safari ndefu ya zaidi ya KM 1450 kwa basi na kutumia zaidi ya saa 22 kufika mwisho wa safari ni ajabu kufikia mchezo mwingine wa ligi bila kupumzika japo kwa saa chache.

Kanali Mbunge alisema, kuwapeleka wachezaji uwanjani kwa mazingira ya namna hiyo, si tu kuwachosha bali ni kuwasababishia madhara makubwa kiafya, kwa hali hiyo akasisitiza kutoipeleka timu uwanjani kesho kucheza na Yanga katika uwanja wa Uhuru, Dar es salaam.

Aidha Kanali Mbunge alisema, mbali na madhara ya kiafya kwa wachezaji, mchezo huo ukichezwa kesho, timu yake haitatoa ushindani wowote kwa timu pinzani kwani, wachezaji wamechoka sana, miongoni mwao wakiwa ni majeruhi ambao hawataweza kabisa kucheza mchezo huo kwa siku ya kesho.

Kanali Mbunge alisema, kuliko kuwachosha wachezaji kwa kuwafanyisha kazi ngumu kama punda bila kupumzika, ni vema wakapoteza pointi kwa kutopeleka timu uwanjani.

Awali mchezo huo uliahirishwa kupisha mchezo wa Yanga wa Kimataifa na kupangwa uchezwe Novemba 10, mchezo huo ulibadilishwa na kupangwa uchezwe Novemba 11, baadae ukabadilishwa tena ukapangwa Novemba 10, hatimaye jana ukabadilishwa na kupangwa uchezwe Novemba 9.

Wema Sepetu 'Me I dont Deal With Washamba'.
Video: Ifahamu siri ya wasanii wa Bongo kukosa tuzo za MTV MAMAs 2016, walichofanya