Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa anayeshughulikia Elimu, Tixon Nzunda amewaagiza Maafisa elimu Maalum na watu wazima kufanyakazi kwa ushirikiano ili kuendana na dira ya nchi inayotaka kuandaa jamii ya watu walioelimika wenye maarifa na ujuzi

Ameyasema hayo wakati akifunga Kikao kazi cha Maafisa elimu Mkoa, Maafisa elimu Maalum na Maafisa Elimu watu wazima, kilichofanyika katika ukumbi wa Mikutano wa Chuo cha Mipango, Jijini Dodoma.

Amesema kuwa haiwezekani kujenga nchi yenye uchumi wa viwanda na watu wanaoweza kushindana bila kuwa na watu wenye maarifa sahihi, ujuzi kamili, kujiamini, wazalendo na wanaoipenda nchi yao kwa ajili ya kuleta mabadiliko ya kweli na maendeleo katika mapinduzi ya viwanda.

Amesema Sekta ya elimu ni kubwa hivyo amewaomba kujenga mshikamano, kufanyakazi kama timu na kusaidiana kwa hali na mali ili kuleta mabadiliko katika sekta ya elimu kwa kuisaidia jamii kuona umuhimu wa elimu nchini

“Acheni majungu, mafanikio ya idara yawe ni ya kila mmoja, msitengeneze makundi ndani ya Idara na ndani ya sekta kwa kuwa sekta ya elimu ni mafanikio ya Taifa, watu walioelimika, wanaojiamini wenye maarifa, ujuzi na wanaoweza kujiamini,”amesema Nzunda

Aidha, ameongeza kuwa katika kuleta maendeleo ya elimu nchini ni lazima kufanyakazi kwa umoja na upendo kwani bila kufanya hivyo hakutakuwa na mabadiliko na kutarudisha nyuma juhudi za Serikali katika kuleta maendeleo kwa jamii na kupunguza changamoto katika sekta ya elimu nchini.

Hata hivyo, amewataka Maafisa elimu nchini kuhakikisha wanasimamia taaluma kuanzia ngazi ya awali, msingi, sekondari na watu wenye mahitaji maalum kwa kusimamia mitaala ya elimu nchini  na kuhakikisha maafisa elimu kata wanatimiza majukumu yao kikamilifu ili kuimarisha elimu kuanzia ngazi ya awali.

 

Dkt. Kalemani atoa onyo kali, 'Nilishasema sitaki visingizio'
Habari kubwa katika Magazeti ya Tanzania leo Agosti 23, 2019