Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt. Allan Kijazi amewataka maafisa Habari  na Mawasiliano Serikalini kuelimisha umma kuhusu umuhimu wa sensa ya Makazi na watu imayotarajia kufanyika Agosti 2022.

Dkt Kijazi alisema hayo mkoani Tanga tarehe 12 Mei 2022 wakati akiwasilisha mada kuhusiana na Sensa ya Makazi  kwenye kikao cha Maafisa Habari, Mawasiliano na Uhusiano Serikalini kinachoendelea mkoani Tanga.

“Ninyi Maafisa Habari mnatakiwa kuelimisha wananchi umuhimu wa taarifa za majengo, na ni kwanini ifanyike wakati huu,” amesema Dkt Kijazi.

Kwa mujibu wa Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, ni vizuri Maafisa Habari wakashiriki vyema katika zoezi hilo kwa kutoa elimu sambamba na kubainisha changamoto na kutoa mrejesho hata kabla ya kuanza kwa sensa ya makazi.

DKt Kijazi alisema, takwimu zitakazopatikana wakati wa zoezi la sensa ya watu na makazi zitaisadia serikali kupanga na kutekeleza mipango yake itakayoleta mabadiliko katika maendeleo ya kiuchumi.

” Naomba nitoe rai kwa wananchi, waiamini serikali yao kwa kuwa zoezi hili la sensa ya watu na makazi litaiwezesha serikali kupanga kutekeleza mipango ya maendeleo itakayoleta mabadiliko katika uchumi vinginevyo hatutapata takwimu sahihi,” amesema Dkt Kijazi.

Aidha, amesema kuwa, lengo la sensa ya watu na makazi pia ni kuiwezesha serikali  kuwa na benki ya taarifa za makazi sambamba na kuhakikisha inakuwa na mikakati ya kujua makazi na kujua miji na  vifaa vilivyotumika.

“Kama nchi lazima tuzingatia mikakati kulingana na takwimu zilizopo na hii ni Sensa ya kwanza ya makazi,” ameongeza Dkt Kijazi.

Kwa upande wake Kamisaa wa Sensa ya Watu na Makazi 2022 Anna Makinda alisema, upo mkakati wa elimu na uhamasishaji kuhusiana na sensa na Maafisa Habari wa Serikali wanalo jukumu la kuhamasisha umuhimu wa sensa.

 “Kila aliyekuwa serikalini lazima azungumzie sensa na maafisa habari ndiyo wenyewe na mkasaidie kuhamasisha hasa katika mitandao ya kijamii  kwa kuwa wanaosoma zaidi mitandao ni vijana,” alisema Makinda.

Makampuni ya Ulinzi yasiyofata utaratibu kufungiwa, PSGP kutatua changamoto
Mashindano ya Kitaifa ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu kurindima Dodoma