Maafisa madini nchini wametakiwa kufuata sheria na kanuni katika utoaji wa leseni za madini ili kuondoa changamoto ya migogoro kwenye migodi ya madini.

Hayo yamesemwa mkoani Morogoro na Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Prof. Shukrani Manya alipokuwa akitoa mafunzo juu ya taratibu za utoaji wa leseni za madini.

Amesema kuwa ni vyema taratibu za utoaji wa leseni za utafutaji wa madini zikafuatwa ambazo ni pamoja na muombaji kubaini eneo linalomfaa kwa utafiti, kujaza fomu ya maombi na kuwasilisha Tume ya Madini.

Aidha, amesema kuwa taratibu nyingine ni pamoja na ombi kupendekezwa na kukubaliwa kupewa leseni, mmiliki wa leseni kuomba ridhaa kwa mmiliki halali wa ardhi ya kuingia kwenye eneo la utafutaji madini..

“Mmiliki wa leseni atatakiwa kuomba ridhaa ya uwekezaji kwenye mamlaka ya serikali za mitaa, mmiliki wa leseni kwa kushirikiana na mamlaka za halmashauri/wilaya kuandaa mpango wa utoaji wa huduma kwa jamii,” amesema Prof. Manya.

Hata hivyo, ameongeza kuwa leseni hutolewa kwa kipindi kisichozidi miaka 10 na Tume ya Madini kwa mtu au kampuni/shirika katika eneo ambalo lipo nje ya eneo la mmiliki wa leseni ya uchimbaji wa madini.

 

Mkataba wa Adidas kusajili wengine Arsenal
Ethiopia yatia saini mkataba wa amani na kundi la OLF