Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad amenena kuhusu uamuzi wa aliyekuwa Mwenyekiti wa chama hicho, Profesa Ibrahim Lipumba kumuandikia barua kutengua uamuzi wake wa awali wa kujiuzulu.

Kwa mujibu wa taarifa ya chama hicho iliyotolewa kwa vyombo vya habari na Mkurugenzi wa Habari na Uenezi, Salim Bimani, Maalim Seif amekanusha taarifa zilizosambaa awali zikimnukuu kuwa amesema ‘Lipumba asahau kuhusu uenyekiti CUF’.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa Maalim Seif amewataka wanachama wa chama hicho kuwa na subira kusubiri uamuzi wa vikao rasmi vya chama kwakuwa masuala ya chama hayaamuliwi na mtu mmoja.

“Hata hivyo, maoni na msimamo wa Katibu Mkuu ambaye yuko Marekani ni kwamba wananchi wasubiri maamuzi ya vikao vya chama vitakavyoamua mambo mbalimbali yanayoendelea na yatakayotokea na vitatangaza maamuzi yake kwa wote,” ilisema taarifa hiyo.

Profesa Lipumba alitangaza kujiuzulu nafasi ya Uenyekiti Agosti mwaka jana baada ya CUF kuridhia uamuzi wa kumuunga mkono Edward Lowassa kugombea urais akiungwa mkono na vyama vya siasa vinavyounda Ukawa kikiwemo chama hicho.

 

Basi Kampuni ya Tahmeed lateketea kwa moto
Video: Seneta na Gavana wazichapa kwenye kikao Kenya