Aliyekuwa mgombea urais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa tiketi ya Chama Cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad amewasilisha rasmi barua yake kwa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) kuhusu uamuzi wake wa kujiondoa katika uchaguzi wa marudio utakaofanyika Machi 20 mwaka huu.

Mkurugenzi wa Mipango na Uchaguzi wa CUF, Omar Ali Shehe amesema kuwa Mwanasiasa huyo mkongwe aliwasilisha rasmi barua yake kwa ZEC, Februari 8 mwaka huu, akiitaka kuondolewa kwenye orodha ya watakaoshiriki uchaguzi huo.

Alisema kuwa katika barua hiyo, Maalim Seif aliieleza ZEC kuwa amechukua uamuzi huo kwakuwa uchaguzi uliofanyika Oktoba 25 ulikuwa huru na haki na kwamba Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jecha Salum Jecha hakuwa na Mamlaka ya Kikatiba kuufuta kama alivyofanya.

Uamuzi huo pia umechukuliwa na wagombea wote wa chama hicho katika nafasi za Uwakilishi na Udiwani, na tayari wote wamekwisha kuwasilisha barua zao ZEC wakiitarifu kuwa hawatashiriki uchaguzi huo.

Vyama 9 ikiwa ni pamoja na CUF, vimetangaza rasmi kutojihusisha na uchaguzi huo huku vyama vinne kikiwemo CCM kikitangaza kushiriki uchaguzi wa marudio.

 

Mwigulu Nchemba afanya ziara ya kushtukiza saa 7 usiku
Mwanamke aliyewanyang’anya Majambazi Bunduki Tarime, aomba azawadiwe Silaha