Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi (CUF), Maalim Seif  amesema kuwa yuko tayari kukamatwa na jeshi la polisi na kufikishwa mahakamani kwa tuhuma za kujitangaza mshindi.

Maalim Seif ambaye alikuwa mgombea urais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar aliyasema hayo jana alipofanya kikao na wajumbe wa mkutano mkuu wa chama hicho, makatibu wa matawi na viongozi wa majimbo.

“Nilisema ni ZEC initangaze kwakuwa nilishinda uchaguzi. Hapo kuna ubaya gani ati? Nilishitakini basi, nasema niko tayari, nishitakini. Nitakuja mahakamani kujitetea, mnamtisha nani… mnamtisha nani hapa?” alisema.

Maalim Seif na viongozi wa chama chake jana waliweka msimamo wao kuwa hawatakubaliana na uamuzi wowote wa kurudia uchaguzi mkuu wala kuwepo kwa serikali ya mpito huku wakiwataka ZEC kuendelea na utaratibu wa kuhakiki matokeo na kumtangaza mshindi.

Pia wametoa wito kwa Rais John Magufuli kuingilia kati suala la Zanzibar na kusaidia kukamilishwa kwa hatua zilizobaki za kumtangaza mshindi.

Mwenyekiti wa ZEC alitangaza kufuta matokeo ya uchaguzi mkuu wa Zanzibar kwa madai ya kuwepo na kasoro nyingi na kwamba uchaguzi mwingine utaitishwa baada ya miezi mitatu.

TP Mazembe Mabingwa Afrika 2015
Kung’arisha Mchele wa Mbeya Kwahatarisha Soko