Rais wa Tanzania, Dkt. John Magufuli amesema baada ya kufanya mazungumzo na aliyekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, enzi za uhai wake Maalim Seif Sharif Hamad alibaini ni kiongozi wa tofauti.

Ametoa kauli hiyo leo Ijumaa Februari 19, 2021 katika ibada ya mazishi ya aliyekuwa katibu mkuu kiongozi, Balozi John Kijazi iliyofanyika katika viwanja wa Karimjee jijini Dar es Salaam.

Maalim Seif alifariki dunia Februari 17, 2021 katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) alikokuwa akipatiwa matibabu na kuzikwa jana Mtamwe wilayani Wete kisiwani Pemba, Zanzibar.

“Maalim Seif alikuwa ni kiongozi wa tofauti sana mwaka 2015 nilipokuwa rais baada ya uchaguzi wa Zanzibar kufanyika ule wa marudio, Maalim Seif aliniandikia barua akiniomba kuja kuniona nilisita kidogo kwamba kwa nini anataka kuja kuniona na wakati hata kwenye uchaguzi hakushiriki, Maalim Seif akaandika tena barua ya pili na baadaye akaandika barua ya tatu.” amesema Rais Magufuli.

“Kila nilipokuwa najaribu kupata ushauri kutoka Zanzibar nilikuwa naambiwa nisubiri nimuache lakini baadaye nikaamua ngoja nimuone Maalim Seif. Alipokuja Ikulu Dar es salaam nilipoanza kuzungumza naye nilimuona mtu tofauti sana na jinsi picha ilivyokuwa imejengeka kwa sababu mazungumzo yetu yalikuwa mazuri sana.”

Magufuli amesema Maalim Seif alimueleza kuwa hakushiriki kwenye uchaguzi wa marudio Zanzibar uliofanyika Machi, 2016 baada ya ule wa Oktoba 25, 2015 kufutwa akisisitiza kuwa licha ya jambo hilo kutokea lakini Zanzibar itakuwa salama na kwamba hatohamasisha fujo.

'VISIT KIDIMBWI' yamponza Manara, atakiwa kuomba radhi
Ihefu FC yazika hofu ya kushuka daraja