Mwanachama maarufu wa chama cha ACT- Wazalendo, Maalim Seif Sharif Hamad amesema kuwa hakuna mtu anayeweza kumziba mdomo wakati akikemea maovu.

Amesema kuwa yeye ni mpinzani, hivyo anawajibu wa kukosoa kwa mujibu wa sheria za nchi.

Ameyasema hayo Mjini Unguja wakati wa uzinduzi wa uchaguzi wa ngome ya wanawake wa chama hicho katika Ofisi ya ACT- Wazalendo, Bububu, mkoa wa Mjini Magharibi.

Aidha, amesema kuwa imekuwa ni kawaida kwa Jeshi la Polisi kuzuia mikutano ya chama hata ile ya ndani ambayo inafanyika  kisheria.

”Haya yanayofanyika yanalengo la kutaka kuturudisha nyuma harakati za kisiasa za chama chetu, nasema hatutakubali kamwe kurudishwa nyuma,”amesema Maalim Seif

Maalim Seif ametoa kauli hiyo mara baada ya kuzuiwa kufanya mikutano katika ukumbi ambao wamekuwa wakifanya mikutano yao ya ndani kwa madai ya kupata vitisho ikiwemo kufungiwa kumbi zao.

Hata hivyo, ameongeza kuwa kumekuwa na visingizio vya kila aina kila wanapokwenda kutoa taarifa kwa Jeshi la Polisi kwa ajili ya kufanya shughuli zao za kisiasa, kwani wamekuwa wakihangaishwa kwa lengo la kuzuia shughuli zao ambazo zipo kwa mujibu wa sheria.

Video: JPM apewa maazimio 30 kuivusha SADC, SADC yapaisha kiswahili Afrika
Mwalimu adaiwa kujiua kwa kunywa sumu