Chama Cha Wananchi (CUF) kimeeleza kusikitishwa na kile kilichokiita mbinu chafu zinazofanywa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, kulazimisha wafanyakazi wa umma na baadhi ya watu kushiriki uchaguzi wa marudio.

Akiongea na waandishi wa habari jana, Katibu Mkuu wa Chama hicho ambaye alikuwa mgombea urais, amesema kuwa wamebaini kuwa wafanyakazi wa umma wameambiwa kuwasilisha vitambulisho vyao vya uraia pamoja na namba za vitambulisho vyao vya kupigia kura ili baada ya kupiga kura, iweze kufahamika nani hakupiga kura.

Akizungumzia msimamo wa chama hicho kuhusu marudio ya uchaguzi huo, Maalim Seif ameeleza kuwa chama chake kiko tayari kufanya mazungumzo na Chama Cha Mapinduzi ili kutafuta maridhiano ya amani lakini alitoa masharti kuwa hilo litafanyika endapo mpango wa kufanyika kwa uchaguzi wa marudio, Machi 20 utasimamishwa.

“Sijui kwa nini CCM wanaogopa sisi tukiongoza. Wana wasiwasi gani, kwamba CUF ikiongoza kutatokea nini? Sisi hatuna ajenda ya kulipiza kisasi,” alisema.

“Hawa wanahisi hawatapata uwakilishi mkubwa, lakini mbona miaka yote tunakuwa na idadi isiyopishana ya wawakilishi?” Alihoji.

Katika hatua nyingine, Maalim Seif alieleza kusikitishwa na uvamizi na vipigo wanavyopata wananchi kutoka kwa makundi ya vijana wanaojiita ‘Mazombi’. Huku akieleza kuwa wanaoshambuliwa ni wanachama wa CUF.

Alisema kuwa alishazungumza na Rais Ali Mohamed Shein kuhusu suala hilo lakini hakuna hatua zilizochukuliwa.

Aliwataka wanachama wa CUF na wananchi kwa ujumla kuendelea kuwa watulivu na wavumilivu ili wasiingie kwenye machafuko kama yaliyotokea mwaka 2000.

 

Video Mpya: Diamond & AKA - Make Me Sing
Waziri Annastazia Wambura Atembelea TFF