Makamo wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Chama cha ACT Wazalendo, Maalim Seif Sharif Hamad, amewataka Wazanzibar walio ndani na nje ya nchi wakubali kuunga mkono maridhiano kwa kuzika historia na majeraha yaliyopita ili kuijenga Zanzibar iliyo bora.

Maalim Seif ametoa wito huo Desemba 8, 2020, wakati akizungumza mara baada ya kula kiapo cha nafasi hiyo mbele ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt Hussein Mwinyi, Ikulu ya Zanzibar.

“Nitoe wito kwa Wazanzibar wote waliondani na nje ya nchi, wakubali kunyoosha na kupokea mkono wa maridhiano, tumeze machungu yanayotokana na uchaguzi, historia yetu imejaa majeraha ya kila aina ni wakati wa kuzika historia hiyo na kushikamana na kuijenga Zanzibar yetu”, amesema Maalim Seif.

Akizungumzia sababu iliyopelekea wao kuingia katika maridhiano na kukubali kuwa Makamo wa Kwanza wa Rais, Maalim Seif amesema kuwa chama cha ACT – Wazalendo kimefikia uamuzi huo kutokana na imani yao kwa Rais Mwinyi pamoja na dhamira safi aliyonayo ya kuwatoa walipokwama na kuibadilisha Zanzibar katika nyanja zote.

“Moja ya yaliyofanya kukubali maridhiano ni imani yetu kwako Rais Mwinyi, vitendo na ishara zako ambazo zimetushawishi kuwa una nia njema na dhamira safi ya kututoa tulipokwama na kuibadilisha Zanzibar yetu katika nyanja zote” amesema Maalim Seif.

“Tumeona wewe Rais Mwinyi tunaweza kufanya nawe kazi, kusikilizana, nia yako njema imefanya tutangulize nchi licha ya yote yaliyojitokeza kwenye Uchaguzi, wenzangu walipokuja na wazo la kuungana niliwaambia wachague damu mpya nipumzike wakanikatalia” ameongeza Maalim Seif.

Hii ni mara ya pili kwa maalim Seif kushikili wadhifa huo ambapo mara ya kwanza ilikuwa mwaka 2010 – 2015 chini ya uongozi wa Rais mstaafu wa Zanzibar, Dkt. Ali Mohammed Shein.

Habari kubwa kwenye magazeti leo, Desemba 9, 2020
Tanzania, Namibia zakubaliana kuimarisha sekta za Uvuvi na Mifugo