Siku mbili za sintofahamu baada ya aliyekuwa mwenyekiti wa Chama Cha Wanachi (CUF) kujiuzulu wadhifa wake siku chache baada ya Ukawa kumsimamisha mgombea mmoja wa urais, zimepelekea chama chake kutoa msimamo wake mapema.

Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad, amesema kuwa chama chake kitaendelea kuwa imara na kusisitiza kuwa kama kuna mwanachama aliyeingia katika chama hicho kwa sababu ya Profesa Lipumba ana uhuru wa kuondoka pia.

Maalim Seif aliyasema hayo jana katika makao makuu ya chama hicho, Buguruni jijini Dar es Salaam. Hata hivyho, alimshukuru Profesa Lipumba kwa mchango wake uliopelekea kuundwa kwa umoja wa vyama vya upinzani uliozaa Ukawa.

“Tunamshukuru sana profesa Lipumba kwani ndiye muasisi wa Ukawa na yeye ndiye aliyekuwa Mwenyekiti wa wenyeviti wa Ukawa, yeye ndiye aliyekaa na wenzake wakakubaliana kumkaribisha Lowassa katika Ukawa,” alisema Maalim Seif.

Aliushangaa uamuzi wa Profesa Lipumba kwa kuwa yeye ndiye wa kwanza kumsafisha Edward Lowassa hadharani na kuongeza kuwa umoja huo utaendelea kuwa imara kwa kuwa ujio wa waziri mkuu huyo wa zamani umeongeza nguvu zaidi itakayowapa ushindi.

“Ukawa umeimarika kwa kumuita Lowassa, kwa hivyo nguvu ya pamoja ya vyama vinavyounda Ukawa ikiungwa mkono na wananchi wote wa Tanzania, nina uhakikika mgombea urais wa CCM, Dk. John Magufuli, Ikuku ya Magogoni hataiona. Nina hakika Ukawa inachukua dola wala si dhamira yetu kurudi nyuma,” alisisitiza.

Moja kati ya sababu alizozitoa Profesa Lipumba wakati anatangaza uamuzi wake wa kujiuzulu uenyekiti wa CUF, alisema Ukawa imeyaacha malengo waliyokuwa nayo awali kwa kuwakaribisha watu ambao awali walikuwa wakiipinga Katiba iliyopendekezwa na wananchi katika Bunge Maalum la Katiba.

Lipumba alitangaza uamuzi wa kujiuzulu wakati ambapo Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Wilbroad Slaa akiwa amepumzika baada ya kutokubaliana na uamuzi wa Ukawa kumkaribisha Lowassa ingawa naye pia alishiriki vikao vyote vilivyofikia maamuzi hayo.

Profesa Lipumba Amuunga Mkono Zitto Kabwe
Everton Wazitosa Man City, Spurs