Klabu ya Mtibwa Sugar imefurahia maamuzi ya shirikisho la soka nchini TFF ya kuruhusu michezo ya kirafiki kuendelea, kabla ya kuendelea kwa mshike mshike wa Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho Tanzania Bara (ASFC).

Juzi Jumatatu Shirikisho la Soka nchini (TFF) lilitoa taarifa la kusimamisha michezo yote ya kirafiki mpaka itakapokutana na klabu za Simba, Yanga, Azam, Transit Camp, Namungo, KMC na Ndanda ambazo zilionekana kukiuka muongozo uliowekwa na serikali, shirikisho hilo na Bodi ya Ligi Kuu kuhusu mwenendo wa mashabiki viwanjani katika kipindi hiki cha janga la virusi vya Corona.

“Hakuna mchezo wowote wa kirafiki ambao utaruhusiwa kucheza bila ya ruhusa ya TFF,” ilieleza taarifa hiyo ya TFF pamoja na kukutana na uongozi wa Simba, Yanga, Azam, KMC na Transit Camp.

Hata hivyo Jana Jumanne baada ya kukutana na viongozi wa timu hizo iliruhusu kuendelea kwa michezo ya kirafiki kwa kupata kibali kutoka TFF ngazi husika

“Tulikubaliana kwamba klabu zitaunda vikundi ambavyo wataviita ‘social distancing agents’ miongoni mwa mashabiki wao. Watahamasishana wenyewe ili kutekeleza yale maagizo ya kukaa umbali unaostahili.

Tumekubaliana kwamba Azam na KMC wataendelea na mechi yao ya kirafiki ambayo wameahidi kwa kushirikiana na wadau mbalimbali itakuwa kama ya mfano wa utekelezaji wa miongozo ambayo imetolewa,” alisema Rais wa TFF, Wallace Karia.

Kocha Mkuu wa Mtibwa Sugar, Zuber Katwila amesema kuwa siku moja kabla ya kufanyika kwa kikao hicho (Jana Jumanne), walikua na wakati mgumu kutokana na umuhimu wa michezo ya kirafiki, ambayo ilidaiwa kusimamishwa na TFF.

“Tunaendelea na mazoezi kama kawaida kujiandaa na michezo yetu ya Ligi Kuu hadi pale tutakaoona tumekaa vizuri.

“Michezo ya kirafiki inasaidia sana wachezaji na pia kocha kujua hali ya vijana wako walivyoimarika,” anasema Katwila.

Naibu waziri wa Afya akutana na madereva malori Namanga
Roger Federer kuonekana tena uwanjani 2021