Maandamano ya wafuasi wa chama kikuu cha upinzani cha Gabon wanaopinga matokeo ya uchaguzi yaliyompa ushindi Rais Ali Bongo Ondimba, yamesababisha vifo vya watu watatu na takriban watu elfu moja wamekamatwa na jeshi la Polisi.

Vurugu hizo zilizuka baada ya kiongozi wa Upinzani, Jean Ping kutangaza kupinga matokeo hayo akidai yamechakachuliwa huku akijitangaza kuwa mshindi halali wa kinyang’anyiro hicho cha Urais.

Rais Ali Bongo na Jean Ping

Rais Ali Bongo(Kushoto)  na Jean Ping

Hata hivyo, Rais Bongo amewataka wananchi kuendelea na shughuli zao kwani wanajua nani aliyeshinda na kwamba wanaofanya vurugu ni kundi dogo lililoshindwa uchaguzi.

“Najua aliyeshinda na aliyeshindwa,” alisema Rais Bongo. “Nani aliyeshinda? Ni watu milioni moja na laki nane wa Gabon ambao tutaendelea nao pamoja. Na nani aliyeshinda? Ni kundi dogo ambalo nia yao ni kuchukua madaraka ili waitumie Gabon badala ya kuitumikia,” anakaririwa.

Waandamanaji wamefanya vurugu kubwa mitaani wakichoma magari na majumba mbalimbali. Walichoma magari nje ya majengo ya Tume ya Uchaguzi ya Taifa hilo na kupelekea moshi kutanda kila mahali.

Tume hiyo ilimtangaza Bongo kuwa mshindi kwa ushindi mwembamba dhidi ya Ping (49.8% dhidi ya 48.2 %).

Umoja wa Mataifa umeomba kurejeshwa kwa hali ya amani nchini humo ili kunusuru wananchi na mali zao.

Free State Stars Waachana Na Mrisho Ngassa
Dully awaponda wanaofanya video nje ya nchi ‘ni ulimbukeni’