Bodi ya Ligi Tanzania Bara ‘TPLB’ imezipa ahuweni klabu za Simba SC na Young Africans, kuelekea michezo ya Mzunguuko wa Kwanza Ligi ya Mabingwa Barani Afrika msimu huu 2022/23.

Young Africans ilitinga hatua hiyo kwa kuwabanjua Mabingwa wa Sudan Kusini Zalan FC jumla ya Mabao 9-0, huku Simba SC ikiwatoa Mabingwa wa Malawi Nyasa Big Bullet kwa ushindi wa jumla wa 4-0.

Katika hatua hiyo Young Africans itaanzia nyumbani Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam kwa kuwakabili Mabingwa wa Sudan Al Hilal, huku Simba SC ikipangiwa kuanza ugenini dhidi ya Primira de Agosto ya Angola kati ya Oktoba 07-09.

TPLB imezipa ahuweni klabu hizo za Kariakoo-Dar es salaam, kufuatia kufanya mabadiliko ya Ratiba ya baadhi ya Michezo ya Mzunguuko wanne wa Ligi Kuu Tanzania Bara, iliyokuwa imepangwa kuchezwa baadae mwezi huu.

Hata hivyo TPLB imetoa sababu tofauti kwa kueleza kuwa michezo hiyo imesogezwa mbele kutokana na Klabu zilizoguswa na mabadiliko hayo kuwa na wachezaji kwenye timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ itakayocheza michezo ya Kimataifa ya Kirafiki dhidi ya Uganda na Libya mwezi huu.

Barua ya TPLB imeeleza: Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) imefanya maboresho ya ratiba katika michezo sita (6) ya Ligi Kuu ya NBC kama ifuatavyo:

1-Mchezo namba 35 KMC FC dhidi ya Mtibwa Sugar FC uliopangwa kuchezwa Septemba 27, 2022 saa 10:00 alasiri katika uwanja wa Uhuru uliopo Dar es Salaam, sasa utachezwa Oktoba 15, 2022 saa 10:00 alasiri katika uwanja wa Uhuru uliopo Dar es Salaam.

2-Mchezo namba 33 Ruvu Shooting FC dhidi ya Coastal Union FC uliopangwa kuchezwa Septemba 26, 2022 saa 10:00 alasiri katika uwanja wa Uhuru uliopo Dar es Salaam, sasa utachezwa Septemba 29, 2022 saa 10:00 alasiri katika uwanja wa Uhuru uliopo Dar es Salaam.

3-Mchezo namba 34 Polisi Tanzania FC dhidi ya Namungo FC uliopangwa kuchezwa Septemba 27, 2022 saa 8:00 mchana katika uwanja wa Ushirika uliopo Kilimanjaro, sasa utachezwa Oktoba 19,2022 saa 10:00 alasiri katika uwanja wa Sheikh Amri Abed uliopo Arusha.

4-Mchezo namba 38 Ihefu SC dhidi ya Young Africans SC uliopangwa kuchezwa Septemba 29, 2022 saa 10:00 alasiri katika uwanja wa Highland Estate uliopo Mbeya, sasa utachezwa Novemba 29, 2022 saa 10:00 alasiri katika uwanja wa Highland Estate uliopo Mbeya.

5-Mchezo namba 36 Kagera Sugar FC dhidi ya Singida BS FC uliopangwa kuchezwa Septemba 28, 2022 saa 8:00 mchana katika uwanja wa CCM Kirumba uliopo Mwanza, sasa utachezwa Oktoba 21, 2022 saa 10:00 alasiri katika uwanja wa Kaitaba uliopo Kagera.

6-Mchezo namba 37 Mbeya City FC dhidi ya Simba SC uliopangwa kuchezwa Septemba 28, 2022 saa 10:00 alasiri katika uwanja wa Sokoine uliopo Mbeya, sasa utachezwa Novemba 23, 2022 saa 10:00 alasiri katika uwanja wa Sokoine uliopo Mbeya.

Sababu ya maboresho haya ni baadhi ya timu zinazohusika na michezo tajwa hapo juu kuwa na wachezaji waliojiunga na timu zao za taifa.

Idara ya Habari na Mawasiliano
Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB)
Septemba 21, 2022.

Ujenzi bwawa la umwagiliaji kusaidia ukuzaji sekta ya Kilimo
Waandamana kupinga mauaji, sheria ya Hijab