Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania, IGP Camillus Wambura amefanya mabadiliko madogo kwa baadhi ya Makamanda wa Polisi ili kujaza nafasi zilizokuwa wazi baada ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama kuteua na kuwapandisha vyeo baadhi ya Maofisa

Mabadiliko hayo yamefanywa Agosti 1, 2022 na baada ya uteuzi uliofanywa na Rais Samia tarehe 20.7.2022 . 

Waliohamishwa ni Naibu Kamishna wa Polisi (DCP) Saleh Ambika kutoka Kitengo Maalumu cha Upelelezi wa Makosa ya Jinai kuwa Naibu Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai ambaye amechukua nafasi ya Faustine Shilogile aliyekuwa akishikilia nafasi hiyo ambaye aliteuliwa na kupandishwa cheo na kuwa Kamishna wa Kamisheni ya Polisi Jamii. 

Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Philemon Kahabi Makungu amehamishwa kutoka Mkuu wa Operesheni mkoa wa Kigoma na kuwa Kamanda wa Polisi wa mkoa huo ambaye amechukua nafasi ya Kamishna wa Polisi Ramadhani Kingai ambaye alipandishwa cheo kuwa Kamishna wa Polisi na Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai. 

Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Janeth Magomi amehamishwa kutoka Kamanda wa Polisi mkoa wa Songwe na kuwa Kamanda wa Polisi mkoa wa Shinyanga, ambaye amechukua nafasi ya Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) George Kyando ambaye amehamishiwa Kamisheni ya Uchunguzi wa Sayansi ya Jinai, Makao Makuu ya Polisi Dodoma. 

Pia, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Alex Mukama ambaye alikuwa Mkuu wa Upelelezi mkoa wa Shinyanga amehamishwa na kuwa Kamanda wa Polisi mkoa wa Songwe. 

UNHCR yashindwa kukidhi mahitaji ya wakimbizi
Halmashauri 100 zatikisa makusanyo ya mapato