Mabalozi mbalimbali wanaowakilisha nchi zao hapa nchini, ‘wamemlilia’ Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad na kumuelezea kwa jinsi walivyomfahamu na yale aliyoyafanya enzi za uhai wake hapa duniani.

Mabalozi hao wamewasili katika Ofisi Ndogo za Wizara ya Mambo ya Nje jijini Dar es Salaam kwa nyakati tofauti kwa ajili ya kusaini kitabu cha maombolezo ambapo mara baada ya kusaini kitabu cha maombolezo baadhi yao wakaelezea walivyoguswa na msiba wa Maalim Seif Sharif Hamad.

Balozi wa Ufaransa nchini Frederic Clavier amesema kuwa ni pengo kubwa kwa Zanzibar na kwa Tanzania pia kwani Maalim Seif alikuwa kiongozi mahiri kwa taifa na aliyekuwa na uhamasisho kwa bara la Afrika.

“Alikuwa mtetezi wa masuala mbalimbali ikiwemo demokrasia na haki, pia katika enzi za uhai wake alikubali kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais kwa Serikali ya Zanzibar ni jambo la kuigwa kwa taifa la Zanzibar na Taifa la Tanzania kwa Ujumla,” amesema Balozi Clavier.

Clavier ameongeza kuwa “Maalim Seif alikuwa kiongozi aliyependa amani, na aliyekuwa mstari wa mbele kupigania maslahi ya nchi yake……lakini pia alikuwa mpenda amani na alikuwa mwanasiasa makini ……..kwa kweli tutamkumbuka daimia, tunamuombea kwa Mungu apumzike kwa amani.”

“Kwa muda mfupi niliomfahamu kwa kweli alikuwa kiongozi mahiri aliyependa amani na umoja hakika pengo lake halitazibika kwa urahisi, Mungu ampumzishe kwa amani,” amesema Balozi wa Finland nchini, Riitta Swan.

Kwa upande wake Balozi wa Kuwait nchini, Balozi Mubarak Mohammed Alsehaijan amesema kuwa Hayati Maalim Sief alikuwa kiongozi mpenda amani na atakumbukwa daima kwa mema aliyoyafanya kwa Wazanzibari na Watanzania kwa ujumla.

Baadhi ya mabalozi waliofika na kusaini kitabu cha maombolezo katika Ofisi Ndogo za Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Jijini Dar es Salaam ni pamoja na Balozi wa Zambia Benson Keith Chali, Balozi wa Finland chini Tanzania, Riitta Swan na Balozi wa Kuwait nchini, Balozi Mubarak Mohammed Alsehaijan.

Wengine ni Balozi wa Pakistani nchini, Mohammad Saleem, Balozi wa Ufaransa hapa chini, Frederic Clavier, Balozi wa Zimbabwe nchini, Luteni Jenerali Mstaafu, Anselem Sanyatwe pamoja na Mwakilishi wa Balozi wa Irani, Mohammad Rezaee.  

Habari kubwa kwenye magazeti leo, Februari 19, 2021
Polisi TZ yalikataa kwata la JKT TZ