Kiu ya wakazi wa Dar es Salaam kupata unafuu katika huduma ya usafiri na kuondokana na kadhia ya foleni imeanza kupatiwa maji ambapo serikali imeingiza mabasi 138 yaendayo kasi yatakayotoa huduma katika jiji hilo.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Meck Sadiki aliyapokea na kuyakagua mabasi hayo 138 yaliyowasili katika bandari ya Dar es Salaam yakitarajiwa kufanya kazi chini ya mradi wa Mabasi yaendayo Kasi (DART).

Mkuu huyo wa mkoa alitumia nafasi hiyo kukanusha taarifa zilizoenea kuwa nauli ya mabasi hayo ni shilingi 900. Alisema bado Mamlaka ya Usafiri wa Ardhi na Maji (Sumatra) bado wanaendelea na mazungumzo na kampuni inayotakiwa kuendesha mradi huo.

“Sumatra, kampuni iliyopewa mkataba wa kuendesha mradi huo kwa muda wa miaka miwili kwa mkataba, pamoja na watumiaji wa huduma hiyo bado wako katika mazungumzo ya kutafuta makubalino ya bei itayotumika,” alisema Mkuu huyo wa Mkoa.

Mabasi hayo 138 ya kisasa yaliyoingizwa Dar es Salaam yanaungana na mabasi mengine mawili yaliyokuwa yamewasilishwa mapema hivyo kukamilisha idadi ya mabasi 140. Mabasi hayo yanatarajia kuanza kutoa huduma kuanzia Oktoba 2 mwaka huu, yakifanya safari zake kutoka Kimara hadi Kivukoni, Morocco – Magomeni-Kariakoo (Fire) hadi Posta.

Mathieu Valbuena Azusha Balaa Stade Velodrome
Hans Poppe: Yanga Jiandaeni Kunywa Supu