Mabingwa watetezi wa ligi kuu Tanzania Bara, Yanga SC wanatarajiwa kusafiri siku ya Jumatano ya wiki hii, yaani kesho kuelekea Mauritius tayari kabisa kwa pambano lao la ligi ya mabingwa barani Afrika dhidi ya wapinzani wao ambao ni Sekho De Joackim.

Msafara wa Yanga unatarajiwa kuwa na wachezaji 21 na viongozi 7 huku mkuu wa msafara akiwa ni Ayubu Nyenzi.

Afisa habari na mawasiliano ya Yanga, Jerry Muro ameelezea juu ya safari hiyo na kujinadi kwamba wapo tayari kwa mapambano huku wachezaji wao wakionekana kuwa vizuri.

“Mimi niseme tu, tupo tayari kwa safari na tunakwenda kupambana. Wachezaji wote wapo vizuri, Thabani Kamusoko yupo vizuri, Mwinyi Hajji Ngwali amerejea.

“Msafara wetu utaongozwa na Ayubu Nyenzi, msafara utakuwa na wachezaji 21 na viongozi 7.”

Yanga haitacheza michezo yake miwili ya Ligi kuu Tanzania Bara dhidi ya Mtibwa Sugar na African Sport ili kupisha ushiriki wao katika ligi ya mabingwa barani Afrika.

Mchezo wa Yanga dhidi ya wapinzani wao, Sekho De Joackim unatarajiwa kuvurumishwa siku ya Jumamosi majira ya saa tisa alasiri kwa saa za Mauritius.

Miyeyusho Na Nassibu Ramadhani Wasaini Mkataba Wa Kupanda Ulingoni
Wanyama Aigharimu Southampton Kwa Adhabu