Mabomu mawili yamelipuka leo Jumanne Novemba 16, 2021 katika Jiji la Kampala nchini Uganda.

Taarifa kutoka Kampala zinasema kuwa bomu moja limelipuka mkabala na Kituo Kikuu cha Polisi katika Jiji la Kampala jingine lililipuka karibu na jengo la Bunge la Uganda.

“Tunachoweza kusema ni kwamba haya ni mashambulizi lakini kuhusiana na aliyehusika, hilo bado ni suala linalochunguzwa,” Naibu Mkuu wa Polisi ya Uganda, Edward Ochom, aliliambia shirika la habari la AFP.

Mripuko uliotokea karibu na kituo cha polisi ulivunja vioo vya madirisha wakati ule wa karibu na lango la bunge ukizisababisha gari kadhaa zilizoegeshwa hapo kuunguwa moto na maeneo yote yapo katikati ya eneo la kibiashara, kwa mujibu wa polisi.

“Tumetuma timu ya uokozi kwenye eneo hilo,” alisema msemaji wa Shirika la Msalaba Mwekundu nchini Uganda, Irene Nkasiita.

Kutokana na milipuko hiyo, Bunge la Uganda limezingirwa na vyombo vya ulinzi na usalama.

Kwa mujibu wa vyombo vya habari nchini Uganda, baadhi ya watu wamejeruhiwa kutokana na milipuko hiyo.

Majaliwa:Uchumi wa Nchi utakuzwa na wawekezaji.
Sabaya afikishwa Mahakamani leo