Watu zaidi ya 28 wameripotiwa kufa na wengine 60 wamejeruhiwa kufuatia tukio la kigaidi la mabomu ya kujitoa muhanga katika uwanja wa ndege wa Ataturk  jijini Istanbul nchini Uturuki. Idadi hiyo ya waliopoteza maisha inahofiwa kuongezeka.

Gavana wa Istanbul, Vasip Sahin amewaambia waandishi wa habari kuwa watu watatu wenye mabomu walijitoa muhanga na kufyatua risasi kisha kufanikiwa kupenya katika maeneo ya uwanja wa ndege na kutekeleza mauaji hayo.

Gavana huyo alieleza kuwa bomu la kwanza lilipuka nje ya uzio katika njia za upenyo na mawili yaliripuka katika maeneo ya geti la kuingilia ndani ya uwanja huo na geti maalum la ulinzi.

Mashuhuda wa tukio hilo wameeleza kuwa waliona watu wengi wakiwa wanakimbia huku wengine wakiwa wanatoka damu nyingi wakijaribu kujiokoa. Takribani magari 46 ya kubeba wagonjwa yaliwasili uwanjani hapo.

Hakuna kundi lolote la kigaidi ambalo limekwisha tangaza kuhusika na tukio hilo.

Uwanja huo wa ndege ni wa 11 duniani kwa kuwa na shughuli nyingi na kupokea abiria wengi kwa wakati mmoja.

Ataturk Airport

Ataturk Airport

 

Unai Emery Avishwa Viatu Vya Laurent Blanc
Serikali yafafanua taarifa za ‘kupima ukimwi nyumba kwa nyumba’