Mkuu wa Wilaya ya Nanyumbu, Moses Machali amesema kuwa amekuwa haonekani kwenye medani za siasa nchini tangu alipoteuliwa na Rais Magufuli akisema kuwa kazi anayoifanya kwa sasa inamnyima nafasi ya kuonekana kwa umma.

Amesema kuwa licha ya kuwa kwenye Wilaya ambayo iko Mkoa wa Kusini ambapo ni ngumu kwa wanahabari kufika kwa ajili ya kutambua changamoto za wananchi lakini amekuwa akifanya shughuli za kila siku ikiwemo kupambana na sakata la zao la korosho kwa kudhibiti kangomba.

“Si kweli kwamba niko kimya sana, tatizo waandishi wa habari hawatutembelei kwa sababu wilaya yangu iko mbali sana kutoka Mtwara Mjini, na hata kama Spika alisema tutumie mitandao ya kijamii kujitangaza kazi zetu, Spika anajua kuna tofauti kati ya kazi za kibunge na Ukuu wa Wilaya.”amesema Machali

Aidha, akizungumzia juu ya sula la mpango wake wa kurudi tena bungeni kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 amesema kuwa hatosema chochote kwasasa kwasababu atakuwa amekiuka utaratibu na misingi ya chama.

Hata hivyo, Moses Machali aliteuliwa na Rais Magufuli, Julai 28 mwaka huu kuwa Mkuu wa Wilaya ya Nanyumbu pamoja na makada wengine waliohama kutoka upinzani na kujiunga na CCM, akiwemo Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mjini, Patrobas Katambi na David Kafulila ambaye ni Katibu Tawala wa Mkoa wa Songwe.

Polisi wanawake wapongezwa jijini Arusha
Majengo ya tume ya taifa ya uchaguzi Congo DR yateketea kwa moto