Wafanyabiashara wadogo maarufu kama ‘Machinga’ wamepigwa marufuku kufanya kazi zao kwenye barabara kuu jijini Arusha.

Akitoa agizo hilo, Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Gabriel Daqqaro amesema kuwa ni kitu cha ajabu kuona barabara za jiji hilo zimegeuzwa kuwa sehemu ya soko la wazi isiyo na mpangilio.

“Serikali haijawahi kuwaruhusu kulaza bidhaa zenu barabarani,” alisema Daqqaro na kuongeza kuwa Serikali imejikita katika kusaidia sekta zisizo rasmi lakini haikuwa na maana kuwa machinga wanaruhusiwa kufanya biashara zao hovyo na kuziba barabara muhimu jijini.

Alizitaja barabara ambazo zinaunganisha eneo maarufu la Friends Corner katikati ya jiji na Levolosi, kama barabara ambazo zimekuwa sugu kwa biashara za wamachinga zisizo na mpangilio na zinazoziba barabara hizo, hususan muda wa jioni.

Mkuu huyo wa Wilaya alieleza kuwa Mamlaka ya Jiji iko kwenye mpango wa kuandaa maeneo maalum kwa ajili ya wafanyabiashara wadogo.

Aidha, aliwataka wafanyabiashara wote wadogo kuhakikisha wamesajiliwa kabla ya kuanza kufanya shughuli zao katika jiji hilo.

Usajili huo unaofanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania utasaidia wafanyabiashara hao kuwa na namba ya utambulisho wa mlipa kodi (TIN number) itakayowawezesha kulipa kodi.

Paraguay yafungua ubalozi nchini Israel
Ajali mbaya yaua maofisa watatu wa TIC

Comments

comments