Serikali imewataka madereva wa malori nchini kuchukuwa tahadhari dhidi ya Virusi vinavyosababisha ugonjwa wa Corona (COVID-19) ikiwa ni pamoja na kuhakikisha wanakula vyakula ambavyo vitalinda kinga zao za mwili.

Rai hiyo imetolewa na waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu  alipozungumza na madereva 800 wa kampuni mbalimbali za malori zinazosafirisha  mizigo nje ya nchi waliofika katika maabara ya  Taifa ya afya ya jamii iliyoko mabibo jijini Dar es Salam kwa ajili ya kupima kama wana maambukizi ya virusi vya ugonjwa wa Corona au la.

“Nimefurahi sana kuwaona mko hapa kwa ajili ya kupima Virusi vya Corona kama mtakutwa hamna maambukizi ya ugonjwa huu mjitahidi kula matunda yakiwemo machungwa, mananasi, malimao,  mboga za majani na  tangawizi hii itawasaidia kinga zenu za mwili kuwa juu. Pia muwapo safarini mnapopata nafasi msisahau kupiga nyungu,’’, amesema waziri Ummy.

Naye  Kaimu Mkurugenzi wa maabara ya Taifa ya afya ya jamii, Ambele Mwafulango  amesema kwa upande wa madereva walioko jijini Dar es Salaam, kwa siku wanawapima madereva 200.

Amesema kwa madereva walioko mikoani kuna utaratibu maalum wa kuchukuliwa  sampuli ambazo zinatumwa Dar es Salaam kwa ajili ya vipimo.

Majibu ya vipimo hivyo yanatoka  baada ya  saa 48 kama madereva hao  watakutwa hawana maambukzi watapewa vyeti ambavyo vinatumika kwa siku 14.

Hatua hiyo itawasaidia kupeleka mizigo nje ya nchi bila kupimwa tena katika nchi wanazokwenda.

“Madereva ambao tunawakuta hawana maambukizi ya ugonjwa wa Corona tunawapa elimu ya kujikinga na ugonjwa huu wanapokuwa safarini siku zote  ’’ ameeleza Mwafongo

Serikali imetenga utaratibu malum kwa ajili ya madereva wa malori wanaosafirisha mizigo nje ya nchi ambao wanafanyiwa vipimo vya ugonjwa wa Corona  kabla ya kusafiri, ili kuwaepusha na usumbufu unaoweza kujitokeza wanapokuwa safarini.

Shule za msingi kufunguliwa Juni 1 - Uingereza
Wasafiri kutoka Brazil marufuku kuingia Marekani