Wakati baadhi ya wasanii waliofungiwa nyimbo zao na Baraza la Sanaa Tanzania (BASATA) wakilalama, msanii wa Tip Top Connection, Madee amesema kuwa adhabu zinazotoleawa na Baraza hilo haziwaathiri wasanii na kwamba ndio sababu hurudia makosa hayo.

Madee amesema kuwa tangazo la kufungiwa kwa nyimbo husika hugeuka kuwa sababu ya kuzipa umaarufu zaidi nyimbo hizo kwani zinakuwa tayari ziko mitaani. Hivyo, badala ya kuwa adhabu inayoumiza huwafanya baadhi ya wasanii kuona ni njia ya kupata ‘kick’.

“Mtu aathiriki na chochote kile, sana sana anakuwa anakikikisha tu kwa sababu utakaposema nyimbo imefungiwa tu basi mtaani washazoea ‘eeh, BASATA wamefungia’. Basi nyimbo inazidi kufanya poa tu mitandaoni,” Madee aliiambia XXL ya Clouds Fm.

Alisema kuwa BASATA wanapaswa kuwa wabunifu zaidi ili adhabu wanazokuwa wanazitoa kwa wasanii ziwe na athari kubwa kwao na kuwalazimu kutorudia tena.

“Unajua unaponipa adhabu mimi ikiniathiri basi utajua baadae mimi sitarudia tena kitu kama kile. Kwahiyo unakuta wanamziki wanafungiwa lakini baada ya miezi miwili wanatoa wimbo mwingine na unawaambia tena umewafungia,” alisema.

Katika hatua nyingine, Madee alisema kuwa amekuwa makini kuhakikisha hatoi nyimbo zenye matusi na maudhui yasiyofaa kwani alishawahi kupata athari kubwa baada ya wimbo wake wa ‘Tema Mate Tuwachape’ kuondolewa kwenye kinyang’anyiro cha Tuzo za Kili ilipokuwa ikiwania tuzo ya wimbo bora wa mwaka KTMA 2014.

Wimbo huo uliokuwa mkubwa mwaka huo uliondolewa pamoja na wimbo wa Snura ‘Nimevurugwa’ kwa sababu za kimaadili, hususan video zao.

Mpoto, washiriki 'Kili Challenge' wafika Kilele cha Mlima Kilimanjaro
Makonda Kuwa Mwenyeji wa Siku ya Mashujaa Dar