Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) imesema Mfuko wa Pesheni kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) ina wadai wengi hivyo kushindwa kujiendesha vizuri.

Mwenyekiti wa kamati hiyo, Naghenjwa Kaboyoka amesema hayo baada ya kuipitia ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya kwa mwaka 2019/20.

Amesema wamebaini shirika hilo ambalo ni muunganiko wa mifuko minne ya hifadhi ya jamii ya GEPF, PPF, LAPF na PSPF bado halijakaa vizuri kutokana na madeni linayodai.

Kaboyoka ameongeza kuwa PSSSF imeweka hatifungani katika Benki ya Maendeleo (TIB) ya Sh86.1 bilioni na dola 111.4 milioni za Marekani, lakini hadi jana benki hiyo imeshindwa kuwalipa. Benki hiyo, alisema haijakaa vizuri hivyo haieleweki kama itaweza kuwalipa ama la.

“Kwa hiyo inalifanya shirika hili lisiweze kufanya kazi zake vizuri, kuna madeni mengine pia. Serikali ilikopa fedha kwa ajili ya kuwekeza katika majengo mbalimbali ikiwamo Udom (Chuo Kikuu cha Dodoma) ambayo fedha yake haijarejeshwa katika mfuko huo,” alisema.

Pia, Kaboyoka amesema kulikuwa na wafanyakazi waliokuwa wanachangia kabla ya mwaka 1999 ambao michango yao ilifika Sh4.6 trilioni lakini fedha zao zilikuwa hazipelekwi kwenye mfuko wa jamii na Serikali ikaahidi kulipa fedha hizo lakini haijafanya hivyo.

Serikali ilikuwa ikidaiwa Sh731.3 bilioni kutokana na mkopo wa ujenzi wa majengo yakiwamo ya Udom na hadi jana deni lilikuwa limebaki Sh231 bilioni ameongeza Kaboyoka

Amesema kamati inahofu kuwa iwapo Serikali haitolipa madeni hayo itaufanya mfuko uyumbe na tathimini ya kujua uhimilivu wa mfuko kama ilivyoagizwa na Bunge mwaka jana, bado haijafanyika.

“Kamati tumeshindwa kujiridhisha kama shirika hili litaweza kufanya kazi kikamilifu kama ilivyotarajiwa maana Serikali ilivyounganisha mashirika haya yaweze kufanya kazi kwa tija lakini hadi leo hatujaona hilo linatendeka,” alisema.

Pia, wameuagiza mfuko huo kuweka mkakati wa kuhakikisha majengo yao yanapata wapangaji likiwamo la Twin Tower lililopo Dar es Salaam na kufuatilia madeni wanayowadai wapangaji wachache waliopo.

Hivi sasa, PSSSF inalipa pensheni za wastaafu kuliko unavyopokea michango kutoka kwa wafanyakazi kutokana na Serikali kutotoa ajira mpya kwa miaka mitano.

Maboresho ya Instagram kunufaisha wengi
Rais Ndayishimiye apokelewa na mwenyeji wake