Zaidi  ya madereva 1,000 wa magari ya aina mbalimbali wamekamatwamkoani Morogoro, kwa madai ya kudaiwa madeni ya faini za makosa mbalimbali.

Kamanda wa Polisi mkoani humo, Fortunatus Musilimu, amesema madereva hao waliokamatwa kwenye operesheni iliyoanza kufanywa na polisi tangu Januari 18 hadi jana, ambapo jumla ya madereva 1,384 wameshakamatwa.

Amesema hapo mwanzo madereva walikuwa wanapaswa kulipa madeni papo hapo wanapokamatwa na makosa, lakini kutokana na kuwapo malalamiko kuwa hawatendewi haki wakaruhusiwa kulipa baadaye.

“Malalamiko yao wengine wanakamatwa wakati hawana fedha kwa wakati huo, na wengine wanapokamatwa wanaenda kulipa vituo vya polisi vilivyo mbali huku wakiwa wanapaswa kuendelea na safari,” amesema.

Aidha amesema kuwa serikali ya sasa ni sikivu ikasikia kilio chao na kuamua kuweka mfumo na utaratibu wa kuwapa siku saba zakuwawezesha kulipa madeni pale wanapokutwa na faini jambo ambalo limeonekana kupuuzwa.

Pia Musilimu amesema jumla ya pikipiki 396 zimekamatwa kutokana na makosa mbalimbali ya usalama barabaraniikiwamo kutovaa kofia ngumu, kubeba abiria zaidi ya mmoja (mshikaki).

Kamanda huyo amesema kati ya pikipiki hizo zilizokamatwa, 354 zimeandikiwa faini, 22 zilipewa onyo (PF.6) na 20bado zipo kituoni baada ya madereva wa pikipiki hizo kukimbia wakati wa ukamataji.

Baraza la Seneti lapokea hati ya mashtaka dhidi ya Trump
Habari kubwa kwenye magazeti leo, Januari 26, 2021