Serikali imetangaza mpango wa kuyapiga mnada madini ya Tanzanite yenye thamani ya shilingi bilioni 2.5 yaliyokamatwa mwaka jana katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) yakitoroshwa kwenda ughaibuni.

Uamuzi wa kuyapiga mnada madini hayo ulitangazwa jana na Kamishna wa Madini, Mhandisi Ally Samaje katika maonesho ya Tano ya Kimataifa ya Madini ya vito yanayofanyika jijini Arusha.

Hivyo, utaratibu huo wa mnada utamuwezesha tajiri au kampuni itakayomudu bei hiyo au kuongeza kiwango kinachowashinda washiriki wengine, kuyamiliki kihalali madini hayo na kuliingizia pato taifa.

Mhandisi Samaje alisema kuwa hivi sasa Serikali iko makini kupambana na tishio la utoroshwaji wa madini na uvushwaji wa madini hayo bila kufuata utaratibu na sheria na haitamhurumia mtu yeyote atakayekamatwa akijihusisha na suala hilo.

“Serikali iko makini na jambo hilo na ikibainika madini yanatoroshwa bila kufuata utaratibu na sheria hakutakuwa na ‘msalia Mtume,” alisema na kuongeza kuwa Serikali inataka kuhakikisha madini yote yanawafaidisha watanzania.

Fidel Castro ajitabiria kifo, atoa hotuba yake nzito
Serikali yaweka wazi Muda wa kutua nchini ndege mpya za Magufuli