Madiwani wa Chama cha Wananchi (CUF) katika Halmashauri ya jiji la Tanga, jana walijikuta wakirushiana ngumi baada ya kugawanyika kuhusu uamuzi wa madiwani 12 kati ya 20 wa chama hicho kushiriki vikao vya Baraza la Madiwani ambavyo awali walivisusia.

Vurugu hizo ziliibuka katika kikao cha ngazi ya wilaya cha chama hicho kilichoongozwa na Mwenyekiti wake wa Wilaya, Rashid Jumbe ambaye aliwataka madiwani hao 12 kutoka nje ya kikao ili wajadiliwe mmoja mmoja kwa kile alichokiita kusaliti msimamo wa chama wa kutoshiriki vikao vya Baraza hilo hadi muafaka utakapopatikana.

Baada ya kutoka na kusubiri kwa muda nje ya ukumbi, madiwani hao waliamua kuingia kwenye kikao hicho kwa nguvu kwa lengo la kumtoa Mwenyekiti huyo wakidai anataka kujenga makundi na kupasua umoja wao, hali iliyozua tafrani mlangoni huku pande mbili zikirushiana ngumi.

Kutokana na tafrani hiyo, Jeshi la Polisi liliwasili katika eneo hilo na kufanikiwa kuwatawanya wafuasi wa CUF waliokuwa wamejaa nje ya ukumbi huo wakishuhudia vurugu hizo huku nao wakiwa wamegawanyika, na kufanikiwa kuzima vurugu hizo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Benedict Wakulyamba amesema kuwa jeshi hilo linamshikilia Mwenyekiti Jumbe kwa mahojiano kuhusu tukio hilo.

Wakati Mwenyekiti (CUF-Wilaya) akipinga uamuzi wa madiwani hao 12 kushiriki kikao cha Baraza la Madiwani kilichofanyika Oktoba 12 mwaka huu, Katibu wa CUF wa wilaya hiyo, Thobias Haule ambaye pia ni diwani wa Mnyanjani aliwaunga mkono madiwani hao akidai kuwa walifanya hivyo kwa maslahi ya wananchi waliowachagua.

”Tukubali kwamba kwa kipindi cha mwaka mmoja tulichokaa bila kushiriki vikao vya baraza kuna mambo mengi ya maendeleo ya wananchi ambayo hayakufanyika, tumeamua kuhudhuria kwa masilahi mapana ya wananchi,” Haule anakaririwa.

Akizungumzia sakata hilo, Mbunge wa Tanga Mjini, Mussa Mbarouk (CUF) aliwataka wanachama wa chama hicho kuwa wavumilivu kwani uongozi uko imara na hautayumbishwa.

CUF ina madiwani 20 kati ya jumla ya madiwani 36 wa Halmashauri ya Jiji la Tanga huku CCM ambayo inashikilia kiti cha U-Meya ikiwa na madiwani 16.

Mvutano ndani ya Halmashauri hiyo unatokana na madai ya madiwani wa CUF kuwa uchaguzi wa Umeya ulikuwa na hujuma na kwamba waliporwa ushindi wao.

Gambo aagiza Posho sh10,000 tu kwa madiwani Arusha, aweka sharti kuipata
Makamba ahamasisha utunzaji vyanzo vya maji na mazingira