Madiwani wa jimbo la Misungwi, jana walitoa tamko rasmi kwa vyombo vya habari wakimtetea kwa nguvu aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga (mbunge wa jimbo hilo) aliyeondolewa na Rais John Magufuli katika nafasi hiyo baada ya kubainika kuwa aliingia bungeni akiwa amelewa.

Katika tamko hilo, Madiwani hao wameeleza kuwa walishangaa kusikia uamuzi huo wa Rais wakiwa na Kitwanga nyumbani kwake Dodoma, kwakuwa walikuwa naye Bungeni na kuzunguka naye katika maeneo mbalimbali ya Mji wa Dodoma na kisha kukaa naye na hakuwa na dalili zozote za kulewa.

“Tulitoka na kuelekea katika Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) kwa lengo la kututembeza maeneo yote ya Dodoma, lakini ilifika jioni wakati tukirejea nyuumbani tukiwa naye, ghafla tukaona habari zikisambazwa kwenye mitandao ya kijamii kuwa Waziri Kitwanga amevuliwa uongozi kwa kuwa alionekana akiwa amelewa,” ilieleza sahemu ya taarifa ya Madiwani hao.

Madiwani hao walitahadharisha kuwa lipo kundi la wafanyabiashara wa dawa za kulevya pamoja na mafisadi na maadui wa Kitwanga ndani ya CCM na upinzani ambalo lilitoa taarifa za uongo kwa Rais Magufuli na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kwa maslahi yao binafsi.

“Tunachokisema ni kwamba waziri Kitwanga hakulewa kama ambavyo imepotoshwa, bali ulikuwa ni mkakati wa kumchafua na kuhakikisha anavuliwa wadhifa wake ili watu hawa waendelee kufanya maovu yao. Mtandao wa dawa za kulevya, pamoja na wale waliokuwa wanamshutumu kwamba amehusika kuondolewa kwao kazini,” walisema na kutaja baadhi ya majina.

Katika moja ya maazimio yao, waliitaka Serikali kutoa ushahidi wa kikemia unaoonesha kuwa Kitwanga alikuwa amelewa alipokuwa Bungeni. Pia, Bunge kuunda kamati maalum kuchunguza tukio hilo.

Kadhalika walituhumu kitengo cha habari cha Bunge kwa kuhusika kuhariri video inayomuonesha Kitwanga akijibu swali ili aonekane kuwa amelewa.

UNAWEZA KUMWACHA AENDE!
Daley Blind: Vyombo Vya Habari Havijamtendea Haki Van Gaal