Madiwani wa halmashauri ya mji wa Makambako mkoani Njombe wamekiri kutokuwa na imani na mkurugenzi wa halmashauri ya mji huo kwa madai ya kwamba ameshindwa kusimamia baadhi ya miradi ya maendeleo tangu afike katika halmashauri hiyo na kusababisha miradi mingi kushindwa kukamilika licha ya kutengewa fedha.

Wamesema kuwa kudorora kwa miradi mingi ya maendeleo ukiwemo wa maji , hospitali ya wilaya, kituo cha afya Lyamkena na stendi ya maroli kumesababishwa na utendaji mbovu wa msimamizi mkuu wa halmashauri kwa kuwa amekuwa akikaimisha mara kwa mara ofisi yake.

“Leo hii ni miezi kumi lakini bado miradi haijakamilika, haya kuna jengo la halmashauri pale tangia mwaka 2014 tumeanza kulijenga pale mwenge ulipita lakini mpaka sasa hakuna kinachoendelea na pesa zipo tatizo ni nini kwa hiyo sisi tunachojua ni usimamizi mbovu na sisi hatupendi kukaa kwenye nyumba za kupanga, niseme kwamba kwa mkurugenzi wangu huyu ninampenda sana lakini kufanya naye kazi ni shida”amesema Lucy Mbogela na Devid tweve

Aidha, akitoa utetezi wake mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Paul Malala amesema kuwa kusuasua kwa miradi hiyo ukiwemo mradi wa hospitali ya wilaya pamoja na jengo la ofisi za halmashauri kunasababishwa na wakandarasi pamoja taratibu za manunuzi na ulipaji wa serikali.

Kufuatia mgongano huo mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Hanana Mfikwa ametoa msimamo wa halmashauri kuhusu mapendekezo ya baraza kwa kutoa muongozo uliotolewa na waziri mkuu juu ya kuwachukulia hatua viongozi wakuteuliwa.

“Waraka unasema halmashauri inapaswa kuelewa kuwa haina mamlaka za kuchukua hatua za kinidhamu dhidi ya mkurugenzi wala kumkataa, badala yake zinaweza kujadili utendaji na mwenendo wa mkurugenzi na kuishauri mamlaka yake ya nidhamu ya ajira ambaye ni waziri mwenye dhamana wa serikali za mitaa au katibu mkuu kiongozi kupitia ofisi ya mkuu wa mkoa kwa hatua zake,”amesema Mfikwa

BASATA yalifungulia shindano la Miss Utalii
Mbunge Mavunde ashiriki Ujenzi wa Zahanati atoa mifuko 100 ya Saruji