Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amemuagiza Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera na Bunge), Uledi Mussa afuatilie malipo ya kiwanja namba 26 block AA eneo la Kikuyu East kilichouzwa na CDA kwa sh. milioni 240 lakini fedha iliyoingia ofisini ni sh. milioni 6 tu.

Agizo hilo limetolewa na Waziri Mkuu leo Oktoba 6, 2016 wakati akizungumza na watumishi na viongozi wa Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu Dodoma (CDA) kwenye ukumbi wa Hazina ndogo mjini Dodoma.

Waziri Mkuu amesema eneo hilo lilipaswa kuwa na kituo cha mafuta na akataka apatiwe taarifa mapema iwezekanavyo, ambapo0 pia amemtaka Katibu Mkuu huyo afuatilie mkataba wa upangishaji wa jengo la CDA ambalo wamepangishwa taasisi ya Tunakopesha Limited kwa madai kuwa mhusika alipewa bure na sasa anataka kulipangisha tena ili apate cha juu.

Majaliwa amewaonya watumishi hao pamoja na viongozi wao waache tabia ya kushirikiana na madalali kuuza viwanja na akawataka wachape kazi wakijielekeza na kasi ya Serikali ya kuhamia Dodoma.

Uongozi wa CDA umetakiwa kuongeza kasi ya upimaji viwanja kwa sababu mahitaji ni makubwa lakini akaonya kuwa wakati zoezi hilo likifanyika, wananchi walionunua viwanja na bado hawajamalizia kuvilipia, wasinyang’anywe kwa kigezo cha kutaka kuwauzia wengine.

“Mimi nataka idadi ya viwanja vilivyopimwa iongezeke. Lakini pia msitumie fursa hii kuwanyang’anya watu wenye umiliki halali eti kwa sababu Serikali inataka idadi ya viwanja vilivyopimwa iongezeke,”  – Waziri Mkuu, Majaliwa

 

Video: Matembezi ya hisani kuhamasisha uchunguzi wa Saratani kufanyika
Daraja La Kwanza Kuendelea Tena Wikiendi Hii