Mikakati ya Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu nchini (HESLB) iliyotangazwa hivi karibuni imesababisha maelfu ya wadaiwa kumiminika katika ofisi za Bodi hiyo na kuanza kulipia madeni yao.

Hatua hiyo imechukuliwa na wafaidika hao wa mikopo ya elimu ya juu ikiwa ni siku chache baada ya Bodi hiyo kutangaza kuunda kikosi kazi kitakachohakikisha kinawasaka wadaiwa hadi majumbani kwao pamoja na kuanika picha zao kwenye vyombo vya habari.

Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi hiyo, Abdul-Razaq Badru amesema kuwa takribani watu 45,000 wameshajitokeza kuanza kurejesha mikopo yao na kwamba ndani ya kipindi cha wiki moja tangu watangaze mkakati huo, watu elfu tatu wamejitokeza na kuchukua hatua stahiki.

“Ukweli ni kwamba, mwitikio ni mkubwa, wengi wanajitokeza kulipa, wiki iliyopita tulikuwa na idadi ya wanufaika takribani 42,000 waliokuja kulipa lakini hadi leo (jana) wameongezeka na kufikia 45,000 na wanaendelea kuongezeka,” Badru anakaririwa na Habari Leo.

Aliongeza kuwa mkakati wa kuanza kuanika majina na picha za wadaiwa sugu wa bodi hiyo uko palepale na kwamba bado wanafuatilia masuala ya kisheria kabla ya kuanza mchakato huo.

Watumishi wa umma wawezeshwa kupata nyumba
Makamba afanya uteuzi wa wajumbe bodi ya NETFUND