Serikali ya Sudan imetangaza hali ya dharura kwa miezi mitatu baada ya mafuriko ya maji kuua zaidi ya watu 100 na kuharibu makazi ya makumi elfu wiki hii.

Mafuriko hayo yamesababishwa na mfululizo wa mvua kubwa, hali iliyosababisha pia kufurika kwa mto Nile zaidi ya kina chake cha mwisho. Kwa mujibu wa Serikali ya Sudan, makazi zaidi ya 100,000 yameharibiwa katika miji takriban kumi na sita. Hivyo, watu zaidi ya 500,000 wamekosa makazi.

Waziri Mkuu wa Sudan, Abdalla Hamdok amesema, “kwa mujibu wa taarifa niliyopewa na Wizara ya Kilimo na Umwagiliaji, kiwango cha maji katika Mto Nile kimekuwa cha juu zaidi kuwahi kutokea tangu mwaka 1912”.

Hamdok amesema kuwa mafuriko ya mwaka huu yamesababisha majanga makubwa na maumivu ya kupoteza maisha na mali katika nchi hiyo.

Kwa mujibu wa Reuters, mafuriko hayo pia yametishia kuharibu sehemu ya kihistoria ya ‘Meroe Pyramids’ ambayo Shirika la Umoja wa Mataifa (UN) la UNICEF limeitaja kama sehemu ya urithi wa dunia.

Meroe Pyramids

Serikali ya Sudan imeomba jumuiya za kimataifa na mashirika ya haki za binadamu pamoja na nchi rafiki kusaidia kupunguza madhara ya mafuriko hayo.

Wakala wa UN wamewasilisha misaada mbalimbali ikiwa ni pamoja na chakula, maji safi na salama; dawa na makazi ya muda (tents).

Naibu Mkuu wa ofisi za UN zinazoshughulikia masuala ya ubinadamu nchini Sudan, Tinago Chikoto amesema kuwa Sudan inahitaji msaada zaidi kutoka kwa mashirika ya UN na taasisi zisizo za kiserikali.

Rais Maduro: Tumemkamata komando wa Marekani
Jela maisha kwa kulawiti mtoto wa miaka minne