Kundi la kigaidi linalojiita Islamic State (ISIS) linasadikika kuhusika na shambulizi la kigaidi katika klabu ya usiku huko Orlando, Florida nchini Marekani na kusababisha vifo vya watu 50.

Mshambuliaji aliyetambulika kwa jina la Omar Mateen, alivamia klabu hiyo inayotambulika kama klabu maarufu ya watu wanaojihusisha na mapenzi ya jinsia moja na kuwafyatulia risasi.

Tukio hilo lilitokea Wikendi iliyopita majira ya saa nane usiku ambapo Polisi waliingilia kati na kufanikiwa kumuua mshambuliaji huyo.

Rais wa Marekani, Barack Obama amesema kuwa Serikali yake haina shaka kuwa tukio hilo ni la kigaidi na la chuki. “Tunajua vya kutosha kuwa hili ni tukio la kigaidi na tukio la chuki,” alisema Obama katika hotuba yake ya Jumapili.

Mwakilishi wa Kamati ya Ujesusi ya Marekani, Adam Schiff alisema kuwa kutokana na muda ambao tukio hilo limetokea (Mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhan) na taarifa wanazopokea inaashiria kuwa tukio hilo lina uhusiano na ugaidi wa kundi la ISIS.

Alisema kuwa tukio hilo limetokea ikiwa ni siku chache baada ya kundi la ISIS katika makao makuu yake Raqqa, kutishia kufanya mashambulizi katika kipindi hiki cha Mwezi Mtukufu wa Ramadhan.

Audio: Gwajima afyatuka tena, amshauri Magufuli aihame CCM, adai amenasa njama
Arusha: Mchungaji anaswa kwa kumbaka muumini akiwa anamuombea