Watu saba ambao majina yao hayajafahamika mara moja wamefariki dunia na watatu kujeruhiwa katika ajali iliyohusisha magari mawili ya serikali na lori moja, majira ya saa 6:30 usiku wa kuamkia leo Jumamosi, Novemba 3, 2018 katika Kijiji cha Mbande, Kata ya Sejeli, Wilaya ya Kongwa mkoani Dodoma.

Katika ajali hiyo, gari lenye namba za usajili STL 6250 Toyota Land Cruiser mali ya Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ikiendeshwa na Dickson Kitanda (42) Mgita, mkazi wa Dar es Salaam ikitokea Dodoma kuelekea Dar ikiwa na abiria sita iliigonga kwa nyuma gari namba T161 CBB/T152 CBB lori aina ya DAF mali ya Z.S Ally mkazi wa Dar iliyokuwa imeharibika barabarani

Inaelezwa kuwa, baada ya ajali hiyo, STL 6250 iligongana uso kwa uso na gari lingine SU 41173 Toyota Land Cruiser mali ya Mfuko wa Taifa wa Hifadhi za Jamii (PSSSF) ikitokea Dar kuelekea Dodoma ikiendeshwa na Peter Elleson Masamu (35) mkazi wa Dodoma ikiwa na abiria watatu ambao ni Elliad Eliyakunda Mdeme (40), Mwanasheria na mkazi wa Dodoma, Vick Elisala Moshi (51) Katibu Muhtasi wa Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF na Abubakar Mjata Ndwaqta (42) Ofisa Takwimu wa PSSSF mkazi wa Kisasa, Dodoma.

Aidha, taarifa za awali zinasema kuwa waliofariki kwenye ajali hiyo iliyotokea katika Barabara Kuu ya Dodoma – Morogoro, ni ndugu sita wa Naibu CAG waliokuwa wakitoka kwenye msiba Chato mkoani Geita, kati yao wanawake wawili ambao ni abiria wa gari STL 6250 T/ Land Cruiser na dereva wa gari hilo la Ofisi ya CAG huku majeruhi wakiwa watatu, abiria wa gari SU 41173 T/Land Cruiser.

Miili ya marehemu imepelekwa katika Hospitali ya Kongwa na majeruhi watatu wamelazwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma. Chanzo cha ajali bado kinachunguzwa.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, RPC Gilles Muroto amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo.

Watu wasiofanya mazoezi hatarini kupata tezi dume
Majaliwa aridhishwa na ujenzi wa SGR