Jeshi la Magereza nchini limetoa ufafanuzi kuhusu uamuzi wa mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph ‘Sugu’ Mbilinyi kuendelea kuvaa nembo ya namba yake ya mfungwa akiwa uraiani.

Jana, Sugu alihudhuria kikao cha 33 cha mkutano wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akiwa amevalia nembo yenye namba yake ya mfungwa ambayo ni 219/2018, hali iliyowafanya wabunge wengi kumfuata, kuiangalia na kuteta naye.

Akizungumzia uamuzi huo, Afisa Habari wa Jeshi la Magereza, Lucas Mboje alisema kuwa jeshi hilo halihusiki na uamuzi wa Sugu kwani wao wameshamalizana naye, hivyo kuendelea kutumia nembo hiyo kunatokana na utashi wake.

“Sisi tumemalizana naye, kwa sasa sio mteja wetu. Huo ni utashi wake mwenyewe kama Sugu,” Mboje anakaririwa na gazeti la Mwananchi.

Sugu ambaye alihukumiwa kifungo cha miezi mitano jela baada ya kukutwa na hatia ya kutumia lugha ya kufedhehesha dhidi ya Rais John Magufuli, aliachiwa kwa msamaha wa Rais alioutoa Aprili 26 kwenye sherehe za maadhimisho ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Akizungumza kwa mara ya kwanza Bungeni tangu Novemba mwaka jana, Sugu aliuliza swali la nyongeza akihoji kuhusu Sheria ya Huduma ya Habari ambayo alidai inakwenda kinyume na Ibara ya 18 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuhusu uhuru wa vyombo vya habari.

Swali lake lilijibiwa na Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Elias Kwandikwa ambaye alimtaka mbunge huyo kukutana na kujadiliana kuhusu changamoto za sheria hiyo kwani Sheria zote hutungwa na Bunge.

 

Ajali mbaya yaua maofisa watatu wa TIC
Video: Vigogo CCM matumbo joto, Sugu asimamisha mkutano Bunge

Comments

comments