Uongozi wa Magereza ya mkoa wa Mbeya umetoa ufafanuzi kuhusu uamuzi wa kumzuia mbunge wa Mikumi, Joseph ‘Profesa Jay’ Haule kuwaona Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph ‘Sugu’ Mbilinyi na Katibu wa Chadema Kanda za Juu Kusini, Emmanuel Masoga walioko mahabusu ya gereza hilo.

Profesa Jay akiwa ameambatana na mkewe Grace jana walifika katika gereza hilo wakitaka kuwaona viongozi hao wa Chadema wanaoshikiliwa kwa tuhuma za kutoa lugha chafu dhidi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli lakini walishindwa kufanikisha kusudio lao.

Akizungumzia hatua hiyo, Mkuu wa Magereza mkoa wa Mbeya, Kamishna Msaidizi Mwandamizi, Paul Kijida amekiri kuwazuia na kueleza kuwa kiutaratibu haikuwa siku ya kuwaona wafungwa.

“Ni kweli walikuja hadi ofisini kwangu lakini taratibu hiziko hivyo. Siku za kawaida kama hizi huwa tunamruhusu mtu aliyempelekea chakula au ataruhusiwa pale mfungwa au mahabusu anaumwa, au mwanasheria wake anaruhusiwa kama tu kuna kitu muhimu,” alisema Kijida.

Alifafanua kuwa siku ya kuwaona wafungwa kwa watu wa kawaida ni Jumamosi na Jumapili pekee na sio vinginevyo.

Jana, Profesa Jay alieleza kushangazwa na hatua ya kuzuiwa akidai kuwa anachofahamu ni kuwa mbunge hazuiwi kuwaona wafungwa, kinyume na kilichomtokea.

Leo, Profesa Jay amefanikiwa kuwaona Sugu na Masoga waliofikishwa Mahakamani na kuzungumza nao kama alivyoahidi jana kuwa hataondoka mkoani humo hadi atimize azma yake.

Video: Mgombea Ubunge wa CUF Kinondoni adai kumuunga mkono JPM
Majaliwa awatoa hofu wakulima wa Pamba