Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli ameeleza sababu za kumtumbua Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Benard Mchomvu na Bodi yake.

Akizungumza jana katika mahafari ya Chuo Kikuu Huria yaliyofanyika Kibaha Mkoani Pwani, Rais Magufuli alisema kuwa Bodi hiyo kwa kushirikiana na Watendaji iliweka fedha za umma kwenye ‘fixed deposit account’ za mabenki binafsi ili kujipatia faida binafsi.

Alisema kuwa zaidi ya shilingi bilioni 26 ziliwekwa kwenye akaunti ya mabenki 8 katika akaunti maalum inayozalisha fedha na kwamba Bodi hiyo ndiyo iliyotoa idhini.

Aidha, Rais Magufuli aliongeza kuwa vitendo hivyo hufanywa na mashirika mengine ya umma kupitia kwa Maafisa Watendaji Wakuu ambao hufanya makubaliano maalum na mabenki, hivyo alitoa onyo kali.

“Kumekuwa na mchezo huu kwa watendaji ‘ma-chief’ executive’ (Watendaji Wakuu) wanazichukua wanaziweka kwenye benki za biashara kwenye fixed deposit accounts kwa mazungumzo ya uelewano kati ya huyo mkuu wa taasisi na mabenki husika,” alisema.

Rais Magufuli pia aliinyoshea kidole Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) kuwa imekuwa ikijihusisha na vitendo hivyo pia ambapo kuna fedha zaidi ya shilingi bilioni 30 kwenye fixed deposit account. Hivyo alimtaka Waziri wa Elimu, Profesa Joyce Ndalichako kulifuatilia na kuchukua hatua.

Novemba 20 mwaka huu, Rais Magufuli alitengua uteuzi wa Mwenyekiti wa Bodi hiyo pamoja na bodi yake lakini hakueleza sababu za hatua hiyo.

Viwango Vya soka Duniani, Brazil Yaipumulia Argentina
Makonda azidi kuwahukumu wenyeviti, amburuza mwingine rumande